Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wameridhia bajeti ya sh. 54,672,085,923 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza mipango mbalimbali.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 0.1 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2024/2025 ya sh. 54,670,587,923. Ongezeko hilo limetokana na ongezeko la makisio ya Mapato ya Ndani.
Hayo yamesemwa Februari 6,2025 na Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Meshack Ikera wakati anasoma bajeti ya halmashauri hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01757640757962134342421.jpg)
“Kwa fedha kutoka Serikali Kuu, ipo mishahara ya watumishi (PE) sh. 36,651,818,904, miradi ya maendeleo (ruzuku) sh. 6,095,443,019, na matumizi ya kawaida (OC) sh. 3,735,774,000.
“Na fedha za Mapato ya Ndani (Own Source), mapato halisi (Own Source Proper) sh. 1,950,000,000, mapato lindwa sh. 963,000,000, na wadau wa maendeleo (Wahisani) sh. 5,276,050,000, hivyo jumla kuu kuwa sh. 54,672,085,923” alisema Ikera.
Ikera amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri inakadiria kupokea sh. 11,761,493,019 kutoka mifuko mbalimbali kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo Mapato ya Ndani ni sh. milioni 780, Serikali Kuu sh. 6,095,443,019, na fedha za nje (Wahisani) sh. 5,276,050,000.
Ikera ameelezea mapitio ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kipindi cha kuishia Desemba 31, 2024, ambapo kwa mwaka huu halmashauri ilitengewa sh. 54,670,587,923 kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri.
“Hadi kufikia Desemba 31, 2024 halmashauri imepokea sh. 31,869,911,450 kutoka katika vyanzo vyote vya mapato sawa na asilimia 58.29 ya makisio. Hadi kufikia Desemba 31, 2024 kiasi cha sh. 27,551,929,808 ikiwa ni sawa na asilimia 86.45 ya fedha zote zilizopokelewa” alisema Ikera.
Ikera alisema kwa mwaka wa fedha 2024/2025, halmashauri ilikisia kukusanya sh. 2,911,502,000, ambapo mapato halisi ni sh. 1,897,502,000 na mapato lindwa ni sh. 1,014,000,000.
“Hadi kufikia Desemba 31, 2024, halmashauri imekusanya sh. 1,545,362,317 ikiwa ni sawa na asilimia 53.08 ya lengo la makusanyo”amesema Ikera.
Ikera alisema kwa mujibu wa Mwongozo
wa mwaka 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto inatakiwa kuchangia asilimia 20 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Desemba 31, 2024, halmashauri imetoa sh. milioni 218 sawa na asilimia 100.43 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250207-wa0229481677104706837170-1024x449.jpg)
“Hali ya utoaji wa asilimia 40 ya Mapato ya Ndani (kabla ya Mwongozo mpya) kwenye miradi ya maendeleo hadi Desemba 31, 2024. Kiasi kilichotengwa sh.1,897,502,000, kiasi kilichokusanywa hadi Desemba 2023 sh. 1,085,384,459, kiasi kinachotakiwa kutolewa (asilimia 40) sh. 217,076,891, na kiasi kilichotolewa sh. milioni 218 sawa na asilimia 100.43” alisema Ikera.
Amesema kwa mujibu wa Sheria, halmashauri inatakiwa kutoa asilimia 10 ya Mapato ya Ndani kwa ajili ya kuwapa mikopo vikundi vya Wanawake (asilimia nne), Vijana (asilimia nne) na Watu wenye Ulemavu (asilimia mbili). Hadi Desemba 31, 2024, halmashauri imepeleka kwenye Akaunti ya Mikopo sh. milioni 105 ikiwa ni sawa na asilimia 96.74.
More Stories
Majaliwa:Mfumo wa Anwani za makazi huchochea upatikanaji wa huduma za kijamii
Serikali:Dawa za ARV haziuzwi,zipo za kutosha
Tanzania kuendeleza mipango ya kidemokrasia kukomesha mzozo na machafuko Congo