February 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ataka wanaCCM wasibweteke kwa mafanikio 

*Alisema hakuna sababu ya kuwabeza wapinzani uchaguzi Mkuu ujao, yeye, Riais Mwinyi , Nchimbi watambulishwa kwa wanachama

Na Joyce Kasiki,Timesmajiraonline,Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na maendeleo yaliyopatikana katika Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,yanauhakikishia umma ushindi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Hata hivyo alisema wanachama na viongozi wa Chama hicho wasibweteke kwa ukubwa wa Chama hicho au kuongoza dola kipindi chote tangu Uhuru.

Dkt.Samia  aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 48 tangu kuzaliwa kwa chama hicho ambayo yameadhimshwa kwa kuwatambulisha wagombea pekee wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia,Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Ally Mwinyi na Mgombea mwenza wa Rais Samia, Dkt.Emmanuel Nchimbi.

“Kutokana na kazi za maendeleo zilizofanyika katika kipindi hiki hali haitokuwa tofauti kwa Serikali zote kwa kuzipa ushindi,hata hivyo tusibweteke ,pamoja na kujiamini kwamba CCM ni Chama kikubwa ,lakini tusibweteke.”alisema Dkt.Samia .

Alisema hakuna sababu ya kuwabeza wapinzani ,bali wanaCCM wanapaswa kupambana na kueleza mazuri yaliyofanywa na Serikali inayoongozwa na CCM huku heshima na amani nchini vikiendelea kulindwa.

Kwa mujibu wa wa Dkt.Samia wakati chama hicho kikiadhinisha miaka 48 ya kuzaliwa kwake ,anawahakikishia wananchi kwamba CCM kimejipanga kuongoza Serikali kwa mafanikio makubwa.

Alisema,pamoja na mafanikio lukuki yaliyopatikana chini ya Serikali ya CCM ,lakini anatambua bado zipo changamoto ikiwemo ya ajira kwa vijana.

Hata hivyo alisema zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuanzisha programu zinazolenga kuwasaidia vijana kama programu ya Jenga Kesho iliyopo Bora (BBT).

“Ajira kwa vijana ni changamoto lakini tumeanza mabadiliko ya Sera ya Elimu nchini Ili vijana elimu yetu iweze kuwanufaisha vijana na fursa zilizopo nchini,”alisisitiza Dkt.Samia

Vile vile alisema Serikali inaendelea na Programu za kuboresha mazingira ya biashara nchini lakini pia kuimarisha eneo la uchumi wa Buluu  ambayo yote kwa pamoja yamelenga kutoa ajira kwa vijana.

Katika hatua nyingine alisema Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) inapaswa kuimarishwa kwani ndiyo inayotoa kesho iliyopo Bora kwa CCM .

“Ni lazima tuwekeze kwa vijana kuwajenga kiitikadi Ili waielewe siasa ya nchi yetu..,kesho salama ya CCM na nchi itahakikishwa kwa vijana kujengewa uwezo ili waweze kupambana kwa hoja.”alisema na kuongeza

“UVCCM iimarishwe kimkakati kwani ni hazina ya CCM ,hivyo ni lazima wajengewe uwezo wapikwe kiitikadi na katika mazingira ya sasa.”

Amewataka  viongozi na wanaCCM kwa ujumla kutembea kifua mbele ,kuongeza wanachama kwani ndiyo mtaji wa Chama chochote cha siasa kwa ajili ya kukipatia ushindi .