*Awa Rais wa kwanza Afrika kupata Tuzo ya Gates Goalkeeper na pia nje ya Taifa la Marekani, ni kutokana na juhudi zake kuboresha afya, elimu
Na Penina Malundo,Timesmajiraonline, Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan ametunukia tuzo ya kimataifa ya Gates Goalkeepers iyotolewa na Taasisi ya Gates Goalkeeper Foundation inayohusika na miradi mbalimbali inayolenga kuboresha afya,elimu na maendeleo ya kijamii hasa katika nchi zinazoendelea.
Kupitia Tuzo hiyo Rais Samia anaandika historia kuwa Rais wa kwanza kwa bara la Afrika kupata Tuzo hiyo ya Kimataifa na pia nje ya Taifa la Marekani.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kupokea Tuzo hiyo, Rais Samia, alisema tuzo aliyopewa jana kuhusu masuala ya afya ya uzazi anaitoa kwa ajili ya wahudumu katika sekta ya afya kutokana na kujitoa kwao na kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Alisema kuongeza idadi ya wataalamu na wabobezi wa magonjwa ya watoto na afya ya uzazi pamoja na utoaji wa huduma za afya ya uzazi bure ni miongoni mwa mambo yaliyofanyika ndani ya uongozi wake na kusababisha kupungua kwa vifo vya mama na watoto.
Rais Samia alisema uboreshaji wa miundombinu ya afya ikiwamo ununuzi wa vifaa na magari ya kubebea wagonjwa, vimechangia mafanikio hayo ndani ya miaka yake minne ya uongozi wa nchi hii.
Alisema tuzo hiyo ya Gates Foundation Goalkeeper itaithibitishia Dunia umuhimu mkubwa kuhusu juhudi na kazi kubwa ambayo ameifanya katika kushughulikia changamoto za kimataifa, hasa katika afya na mengineyo.
Tuzo hiyo inaithibitishia Dunia namna uongozi wa Rais Samia unavyotambulika katika kutekeleza sera na mipango inayolingana na malengo ya Bill & Melinda Gates Foundation, hasa katika kuboresha matokeo ya afya na elimu nchini Tanzania, kuonyesha mchango wake mkubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa vitendo, kudhihirisha namna uongozi wake unavyoacha alama na kuleta mapinduzi makubwa kwa maisha ya Watanzania, hususan katika maeneo ya afya ya mama na mtoto, upatikanaji wa elimu, na kupunguza umasikini.
Pamoja na kuchochea viongozi wengine na wadau mbalimbali nchini Tanzania na maeneo mengine kuweka msukumo na kipaumbele kwenye mipango muhimu kama afya na mingine na itasaidia pia kuleta fursa nyingine zaidi ikiwemo Msaada.
Aidha, kuendelea kuzidi kutambuliwa huku kutaongeza na kuzidi kuing’arisha taswira ya Tanzania kimataifa, na hatimaye kuvutia ushirikiano zaidi, misaada na kupata miradi ya ziada ya maendeleo kwa Nchi yetu.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango alisema kwa mara ya kwanza Rais Samia anaweka historia ya pekee kuwa Rais wa kwanza katika Bara la Afrika kupata Tuzo hii ya Kimataifa,hii ikionesha ni juhudi kubwa zinazofanywa na serikali yake.
Alisema tuzo hii ni udhibitisho wa kuipiga hatua katika utoaji wa afya ,kukuza maendeleo na kujenga Tanzania yenye malengo.”Tuzo hii imetambua safari ya nchi yetu kuelekea katika kufikia maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa.
”Tunaposherekea mafanikio haya tunamuomba Mungu ampe umri mrefu Rais Samia pamoja na mambo mengine kuweza kuinua usawa katika utoaji wa huduma ya afya kuendeleza jitihada za kimataifa za kupambana na changamoto mbalimbali na kuendelea kutembea kifua mbele katika taifa ambalo linatoa huduma bora za afya,”alisema.
More Stories
Mapambano dhidi ya Marburg waandishi watakiwa kuelimisha jamii
Wajawazito 140, wapatiwa vifaa vya kujifungulia
Wasanii wazidi kumiminika JKCI ofa ya Rais Dkt. Samia