Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Wataalamu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Uhifadhi wa Mazingira na Maendeleo ya Kiuchumi la EMEDO ambalo linalojihusisha na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria wamekutana jijini Dodoma kwa lengo la kujadiliana namna ya kuendelea kushirikiana katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
Kikao kati ya TMA na EMEDO kimefanyika Februari 4,2025 kwenye Ofisi za TMA Makao Makuu,Jijini Dodoma ambapo yamefanyika majaribio ya matumizi ya kifaa maalumu cha usambazaji wa taarifa za hali ya hali ya hewa “Electronic Weather Board”, ambacho kitawasaidia wavuvi na watumiaji wa Ziwa Victoria kwenye kisiwa cha Goziba kuona utabiri wa hali ya hewa unaotarajiwa katika Ziwa kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi ili kuokoa maisha na mali.
Akizungumza katika kikao hicho,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt.Ladislaus Chang’a ameushukuru uongozi wa Shirika la EMEDO kwa ushirikiano unaoendelea kati ya Taasisi hizi wenye lengo la kusambaza taarifa na elimu ya matumizi sahihi ya taarifa zitolewazo na TMA katika maeneo ya ziwa Victoria.
“Haya ni mambo muhimu sana tunapaswa kufanya ili kuoanisha shughuli zetu na maono ya kimkakati na kuleta thamani kwa kile tunachofanya. Nimevutiwa sana na ushirikiano huu kwa sababu tunataka kila mmoja wetu kuchangia katika kufikia maono ya Taifa. Kwa mfano, kuimarisha hatua za kijamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa Duniani “.Amesema Dkt.Ladislaus Chang’a
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EMEDO, Editrudith Lukanga, ameishukuru pia Mamlaka kwa ushirikiano huu na kusema kuwa TMA imekuwa ikitoa wataalamu wake katika kutoa mafunzo kwa jamii na pia kutoa utabiri wa hali ya hewa, jambo ambalo limekuwa na manufaa kwa jamii.
More Stories
EWURA yatangaza bei kikomo za mafuta
Fainali Khimji cup kufanyika Februari 7,2025
Idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa hospitali Mnazi Mmoja yaongezeka