*Ni lile la Kariakoo lililoua, ataja mazito yaliyobainika, lilikuwa na tani 800, wakati uwezo wake tani 250, sasa kukabidhiwa ripoti Tume ya Majaliwa
Na Reuben Kagaruki,Timesmajiraonline
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameanika somo ambalo Serikali imejifunza kutokana na kuporomoja kwa jengo la ghorofa Kariakoo jijini Dar es Salaam mwaka jana na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Aidha, Rais Samia amesema tukio hili liwakumbusha na kuwafundisha mambo mengi sana kuhusu umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuhakikisha wanakuwa na utayari wa kukabiliana na dharura wakati wote.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia aliyasema hayo Ikulu, jijini Dae es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa chakula cha mchana alichowaandalia walioshiriki zoezi la uokoaji kufuatia kuporomoka kwa ghorofa hilo.
Rais Samia alisema wamepata somo jinsi biashara inavyoendeshwa Kariaboo, kwani jengo hilo lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 250 za mizigo, lakini wakati linaporomoka lilikuwa na tani 800.
“Kwa hiyo kwa vyovyote vile linsingeweza kuhimili na hili ni jengo moja nina uhakika majengo mengi yaliyoko Kariakoo yako kwenye mfumo huo huo.
Utanuzi wa majengo, uongezaji wa nafasi unafanywa kwa msingi ule ule uliokuwepo mwanzo, tunarefusha juu, tunachimba chini , lakini kwa msingi ule ule uliokuwepo mwanzo,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema somo la pili ambalo wamepata ni la usimamizi wa ujenzi ili kuhakikisha viwango vya ujenzi vinafuatwa.
“Kwa wale walioliona jengo lile unaona kabisa mchanga ni mwingi kuliko nondo na saruji, kwa hiyo hilo ni somo jingine ambalo tumepata,” alifafanua Rais Samia.
Alitaja somo jingine ambalo wamepata na yeye aliona kwa haraka haraka na pengine kwa wakati ule ndilo lilileta mzozo kwa wafanyabiashara ni mali inayofichwa mle ndani na pengine bila kulipiwa kodi.
“Jengo hilo limetufunulia mambo mengi na sidhani kama zile tani 800 za mizigo zililipiwa kodi .
“Na ndiyo ulikuwa ugomvi mkubwa wa TRA kupeleka watu kufuatilia maghala ndani ya Kariakoo, kwa hiyo hilo ni somo lingine ambalo tumelipata,” alisema Rais Samia.
***Mipango ya Serikali baada ya somo hilo
Rais Samia alisema kawaida ya binadamu baada ya kupata somo anakuwa na mpango wa baadaye.
Alitaja mipango ya Serikali ya baadaye kuwa; Moja kuhakikisha uwepo wa vifaa rasilimali na utaalamu unaohitajika ili kukabiliana na maafa zaidi.
“Tunashukuru sektaa binafsi ilijitoa, lakini vitu hivyo (mitambo) Serikali ilitakiwa tuwe navyo katika kitengo chetu cha maafa au idara ya uokozi, kwa hiyo tumesoma somo letu tutahakikisha maeneo hayo tunayaimarisha na kuyapatia vifaa vinavyotakiwa,” alisema Rais Samia.
Jambo la pili alilosema Rais Samia ni kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mahafa ikiwemo mifumo ya tahadhari ya mapema na kujengea uwezo timu za kamati usimamizi wa maafa katika ngazi mikoa na wilaya.
Alitaja lingine kuwa ni kuhakikisha viwango vya ujenzi vya ubora vinazingatiwa ipasavyo na taratibu za ukaguzi wa majengo zinaimarishwa , sheria za ujenzi zinafuatwa na rasilimali za kifundi zinapatikana kwa ajili ya kusimami sekta hiyo.
***Majibu hoja za Mwenyekiti wa wafanyabiashara
Rais Samia alitumia fursa hiyo kutolea majibu changamoto zilizoainishwa na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo.
Rais Samia alisema kwamba pamoja na mipango hiyo ya baadaye, mwenyekiti wa wafanyabiashara Kariakoo kuna mambo ambayo alieleza kama changangoto wanapoenda kuifanya Kariakoo kuwa ya saa 24.
Rais Samia alisema la kwanza ni ushindani usio sawa kati ya Watazania wenyewe. “Na hili nililisema nataka niliseme tena, kusiwepo upendeleo wa wafanyaiashara, wote walipe kodi sawa,” alisema.
Pia, Rais Samia alikemea wageni kufanya biashara sawa na inayofanywa na wenyeji .” Kuna kipindi nilirushiwa clip, mgeni anapigana na mwenyeji Kariakoo, nikauliza kwa nini wanampiga mtu wa watu, wakasema huyo mmachinga wameshindana katika biashara zao.
Haiwezekani mgeni akawa mmachinga, vijana wetu watafanya nini? Waziri simamia suala hilo.” Alielekeza Rais Samia. Maelekezo hayo yalielekezwa kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo.
Suala jingine ni suala la barabara kuwa fiinyu kwa sababu ya wamachinga kuziba njia, huku wengine wakiwa wamejenga maduka humo ndani.
Rais Samia alisema amenongonezwa na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kuwa hilo ni moja kati ya mapendekezo ya Tume iliyoundwa kuchugunza maghorofa ya Kariakoo, hivyo anawaomba watakapokuja kutekeleza yale mapendekezo ya Tume, basi washirikiane.
Jambo la pili alilosema Rais Samia ni kuwa Dar es Salaam kuna mradi wa DMDP ambao kati ya sera za DMDP wamejipanga kujenga soko kama la Kariakoo eneo la Jangwani ana uhakika wamachinga watahamishiwa soko la Jangwani ili wafanye biashara zao kwa uhuru.
Kuhusu suala la mwenyekiti kumualika Rais Samia Samia kutembelea Kariakoo kwa mara ya pili, hapo aliweka rekodi sawa akisema.
“Mwenyekiti amenialika Kariakoo kwa sababu nimeenda mara moja, Nilienda Kariakoo kwa mara ya kwanza kutembelea wafanyabiashara siku mbili baadaye soko mkalichoma moto.”
Alisema walichoma moto soko hilo kwa sababu alisema changamoto zilizokuwepo na mambo yaliyokuwa yakifanyika ndani ya soko.
“Kwa hiyo ili kuficha yaliyokuwa yakifanyika ndani ya soko mkaamua kulitia moto, hiyo ilikuwa ziara yangu ya kwanza, lakini kwa ujasiri nikasema nalijenga tena na nitalijenga vizuri ili biashara ziendelee,” alisema na kuongeza mara ya pili aliende Kariakoo kutoa pole kwa yake yaliyotokea na mara ya tatu atakwenda kufungua soko jipya la Kariakoo.
Aliwaomba wafanyabiashara na Serikali kushirikiana katika maeneo yote ya miundombinu na ya ulipaji kodi, kwani kodi ndizo zinaendesha yanayofanyika ndani ya nchi.
***Tume ya maghorofa
Rais Samia aliongeza kwamba kama alivyosema Waziri Mkuu aliagiza iundwe kamati ya kuangalia majengo mengine ya Kariakoo.
“Amesema Tumei imemaliza kazi nitawapangie siku ya kuwasilisha na kama nilivyosema taarifa hii itakuwa wazi tutaitoa kwa wananchi wetu ili waelewe mambo yaliyopo pale (Kariakoo),” alisema Rais Samia.
***Pongezi
Rais Samia alisema pamoja na ushiriki wa vijana wa vyombo vya ulinzi na usalama, lakini wanatambua mchango wa watu mbalimbali, sekta binafsi waliotoa michango mbalimbali ikiwemo gesi, maji, mitambo ya kusafisha eneo eneo.
Lakini pia alisema wanawashukuru waliotoa huduma za bure za matibabu, viongozi wa dini waliwaombea waliopoteza maisha,
Rais Samia alimpongeza waziri mkuu na watendaji wote wa serikali kwa uratibu wa zoezi hilo.
Alisema anatambua mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama, kwani mbali ya uokoaji kuna mambo mengine walifanya ili zoezi hilo liende salama.
Alisema Watanzania wanajivunia vyombo vya ulinzi na usalama vyenye maadili, weledi na upendo mkubwa kwa wananchi.
“Tunavishukuru sana na tunawapongeza kwa kazi kubwa za kizalendo wanazozifanya,” alisema.
Pia alishukuru wataalam mbalimbali, wahandisi, madaktari, wauguzi wanasaikolojia kwa kusaidia kuleta suluhisho la kitaalam katika kila hatua ya uokoaji.
“Alisema hapa ndugu yetu aliyenusuriwa, alisema kwamba waliponusuriwa hali ilikuwa mchanganyiko hawajatulia, lakini wataalam wa saikolojia, mdaktari na wauguzi walifanyakazi kubwa sana na leo tunashukuru sana,” alisema Rais Samia na kuongeza;
“Tunashukuru hospitali zote zilizosaidiana nasi katika jambo hili.”
Rais Samia alisema licha ya kuokoa maisha ya watu, lakini Serikali ilikuwa na jicho kali kuokoa mali za wafanyabiashara waliokuwa kwenye jengo hilo.
“Na tushukuru mali tulizoweza kuokoa, zimeokolewa zimekabidhiwa kwa watu, fedha, nguo na mambo mengine na pamoja na changamoto walioeleza waathirika, Serikali itasimamia ili biahsara iweze kuendelea,” alisema Rais Samia.
*** Chakula
Rais Samia alisema aliandaa chakula cha mchana kwa niaba ya ya waliosiriki tukio la uokoaji la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, lakini kuwashukuru Watanzania wote, walioshiriki kwenye uokoaji wakati wa mafuriko ya Rufiji na maporomoko ya Manyara.
“Kwa hiyo ni shukrani zangu ni kwa wote walioshiriki kufanya wokozi kwenye matukio hayo na tunamuomba Mwenyezi Mungu awaweke mahali pema waliofariki kwenye matukio hayo,” alisema Rais Samia.
More Stories
Waislamu wamuombea dua Rais Samia,wasisitiza umoja
Wanachama CCM Kata ya Rujewa wajitokeza kufanya usafi kituo cha afya
TAKUKURU yadhibiti zaidi ya milioni 360