Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Kaliua
Serikali imepeleka kiasi cha milioni 500, shule ya sekondari Mkindo,Tarafa na Jimbo la Ulyankulu, wilayani Kaliua mkoani Tabora kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 4 na matundu 10 ya vyoo ili kuboresha miundombinu ya shule hiyo na kuwezesha watoto wengi kukaa shuleni.
Wakizungumza na Timesmajira Online kwa nyakati tofauti,wananchi Tarafa ya Ulyankulu, wameeleza kuwa Tarafa hiyo ilikuwa na shule chache na miundombinu hafifu lakini kwa sasa Serikali imeboresha miundombinu ya elimu katika vijiji na Kata zote.
Mkazi wa Kata ya Ichemba ambaye ni Mkuu wa shule ya sekondari Mkindo,Annaemmy Mazigo,amesema,Serikali imeipa sekta ya elimu kipaumbele kwa kutenga bajeti ya kutosha ambapo shule hiyo imepokea kiasi cha milioni 500.
‘Kujengwa kwa mabweni haya kumeleta ari na hamasa kwa watoto wa kike na kiume, kupenda shule, hata utoro sasa hivi umepungua na kila mtoto anasoma kwa bidii ili aweze kutimiza ndoto zake,” ameeleza.
Mkazi wa Tarafa hiyo Ashura Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mwongozo, amedokeza kuwa vijiji na Kata nyingi katika Jimbo la Ulyankulu,vilikuwa havina shule za msingi wala sekondari lakini sasa shule zimejengwa.
Amesema Serikali,imepeleka zaidi ya sh milioni 360,mwaka wa fedha uliopita ili kujengwa shule mpya ya msingi Langoni,katika Kijiji cha Ibambo Kata ya Mwongozo ili kupunguza mrundikano wa watoto katika shule ya Ibambo.
Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu,Rehema Migira, amesema Serikali imewapatia mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, mabweni, madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 4 ya utawala wa Rais Samia,Kata zote 15 za Jimbo hilo zimepata shule za sekondari na shule za msingi zimeendelea kujengwa katika vijiji vyote ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt.Gerald Mongela, ameeleza kuwa wakazi wa Tarafa hiyo na Wilaya nzima ya Kaliua,wanajivunia mambo yaliyofanywa na Rais Samia kwa kuboresha huduma za kijamii katika sekta zote.
More Stories
Rais Samia azitaka Wizara husika kusimamia sera ya elimu
Sababu za matukio ya ukatili zatajwa
Upungufu wa maji Mji Korogwe, HTM waeleza mikakati yao