February 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Upungufu  wa maji Mji Korogwe, HTM waeleza mikakati yao

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

KUTOKANA na athari za kipindi hiki cha kiangazi, upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Korogwe uliopo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga umeathirika kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa sasa, uzalishaji wa maji umepungua kutoka lita 5,523,000 hadi kufikia lita 3,866,100 kwa siku.

Hali hiyo inafanya mahitaji ya maji ambayo ni lita 6,289,000 kwa siku, kushindwa kutimizwa ipasavyo. Matokeo yake, kiwango cha uzalishaji wa maji kimepungua kutoka asilimia 88 hadi 62, na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Hayo yamesemwa Januari 30,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe.

Kaimu Meneja Huduma kwa Wateja Ally Mbuyu akisoma kwa niaba ya Mhandisi Mgaza, alisema kutokana na changamoto hiyo jitihada mbalimbali zinafanywa na HTM pamoja na Serikali kuona wananchi wanapatiwa maji ya kutosheleza kutokana na mipango ya muda mfupi na mrefu.

“Moja ya changamoto, ni upungufu wa maji katika vyanzo vya Mbeza na mashindei, na vimefanya uzalishaji wa maji kuwa mdogo na mgao wa maji katika Mji wa Korogwe. Uwezo mdogo wa kuhifadhi maji ukilinganisha na mahitaji ya maji yaliyopo kwa sasa. Uchakavu wa miundombinu iliyojengwa miaka ya 1950 ambayo haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote hasa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo ya katikati ya mji.

“Sasa,mipango ya muda mfupi ni kutumia vyanzo vya visima virefu vya Mbeza mawe, Mtonga na Kwasemangube kwa ajili ya uzalishaji wa maji ili kuimarisha hali ya huduma ya maji katika mji wa Korogwe. Kuboresha miundombinu ya kusambaza maji kwa kulaza bomba lenye urefu wa kilomita
24.9 katika Mji wa Korogwe. Kuendelea kuongeza mitandao ya mabomba katika maeneo ya Mji wa Korogwe ambayo hayana huduma kabisa ya maji kwa kutegemeana na upatikanaji wa rasilimali fedha” alisema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza alisema mipango ya muda mrefu  ni ya ujenzi wa mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha Mto Ndemaha, ambapo litajengwa dakio na  kulaza bomba kuu lenye urefu wa kilomita 21. Kutekeleza ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kujaza lita 2,000,000 eneo la Kwamkole.

Kutekeleza ujenzi wa Nyumba ya Maabara na vifaa vyake (Laboratory House & Laboratory Facilities) katika eneo la Kwamkole. Kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya kusafisha, kuchuja na kutibu maji (Water Treatment Plant) kwa ajili ya kuhakikisha maji yanawafikia wananchi yakiwa safi na salama tofauti na ilivyo hivi sasa.

“Utekelezaji wa mradi wa Miji 28, ambapo Mji wa Korogwe ni moja ya miji itakayonufaika na mradi huo. Hadi sasa mkandarasi yuko eneo la mradi anaendelea na ujenzi katika maeneo mbalimbali ya mradi, ambapo anaendelea na ujenzi wa dakio la maji (Water intake), Ujenzi wa Chujio (Water Treatment Plant), ulazaji wa mabomba, ambapo mpaka sasa amelaza jumla ya kilomita 121.088 kati ya 188, na ujenzi wa matenki manane (8) katika maeneo tofauti”amesema Mhandisi Yohana.

Mhandisi Mgaza amesema shughuli zilizotekelezwa ni kuendelea na ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 2,000,000 katika eneo la Kwamkole kwa kutumia Mkandarasi KGG Investment Ltd kwa gharama ya sh. 962,299,347, ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia hatua ya kujenga kitako cha tenki. Kuendelea na ujenzi wa Nyumba ya Maabara na vifaa vyake (Laboratory House & Laboratory Facilities) katika eneo la Kwamkole kwa kutumia Mkandarasi Greens Construction Ltd kwa gharama ya sh. 331,436,205, ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia hatua ya umaliziaji.

Ujenzi wa mradi wa Ndemaha (Ujenzi wa dakio na mtandao kutoka chanzo hadi tanki lenye lita za ujazo 2,000,000 – Kwamkole) kwa kutumia Mkandarasi Nyangoso Interlife Solution (T) Ltd kwa gharama ya sh. 1,818,080,280, ambapo mpaka sasa Mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na ujenzi wa dakio la maji katika hatua ya umaliziaji.

Ujenzi wa miundombinu ya kusafisha, kuchuja na kutibu maji (Water Treatment Plant) katika eneo la Kwamkole kwa kutumia Mkandarasi, Tumaini Civil Works Ltd kwa gharama ya sh. 1,048,033,984, ambapo mpaka sasa Mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na hatua za uchimbaji wa msingi wa chujio la maji. Ukusanyaji wa Maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji na maunganisho mapya.

HTM imepewa majukumu ya kuhudumia eneo lote la kiutawala la Halmashauri ya Mji Korogwe lenye jumla ya kata 11, mitaa 29. Kwa sasa HTM inatoa huduma ya maji kwenye maeneo hayo kwa kutumia vyanzo mbalimbali isipokuwa mtaa mmoja tu wa Mahenge ambao kwa sasa kuna mradi wa maji unaoendelea kujengwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Halmashauri ya Mji Korogwe ilikuwa na watu wapatao 86,551. Zaidi ya wakazi wapatao 70,971 sawa na asilimia 82 ya wakazi wote katika Mji wa Korogwe wanapata huduma ya maji.

“Mamlaka inahudumia wakazi wa Korogwe kutoka kwenye vyanzo vya maji vya Mto Mdogo wa Mbeza, Mto Mashindei, Mto Pangani (eneo la Old Korogwe na Mgombezi) na visima virefu sita (6) vilivyopo maeneo ya Majengo, Kwasemangube, Mbeza mawe, Manzese, Kwameta na Kwakombo. Miundombinu ya utoaji wa huduma ya maji inajumuisha vyanzo, matenki 15 yenye jumla ya mita za ujazo 3,100 (lita za ujazo 3,100,000), na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 183.95″amesema Mhandisi Mgaza.