Ashura Jumapili, TimesMajira Online,Bukoba
Ufahamu mdogo, imani za kishirikina,ulevi wa kupindukia pamoja na utandawazi,imeelezwa kuwa chanzo cha matukio ya ukatili,huku waathiriwa wa vitendo hivyo wakitajwa kuwa watoto kati ya miaka 12 hadi 16.
Hayo yamebainishwa Januari 30,2025 na Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kagera,Ajuaye Bilishanga,wakati akitoa mada juu ya ubakaji na ukiukwaji wa maadili,katika wiki ya sheria mkoani hapa.
Bilishanga,amesema familia ya muathirika wa kitendo cha ubakaji au ulawiti,inapoingia kwenye makubaliano na familia ya mtuhumiwa nje ya Mahakama wanamalizana.
“Wakishafanya hivyo,sisi tunaosimamia haki inakuwa ni ngumu kufikia yale malengo ili myuhumiwa aweze kuadhibiwa,pia muathirika wa tukio la ubakaji anaweza akajificha na kuacha kuhudhuria mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi,ama akilazimishwa sana anageuka kwa lengo la kumlinda mtuhumiwa ili asikabiliane na kifungo,”amesema na kuongeza:
“Sheria inasema lazima udhibitishe bila kuacha shaka lolote na kama muathirika amesema amemsahau au siyo yeye, Mahakama inakuwa haina kitu kingine zaidi ya kumwachia mtuhumiwa na anapoachiwa akirudi kwenye jamii anaendelea na vitendo hivyo,”.
Akizungumzia suala la imani za kishirikina amesema,kuna watu wamekuwa wakidanganyana kuwa akibaka mtoto mdogo atakuwa tajiri,wengine wamefikia hatua ya kuwaingilia watoto wao, mama zao na wakati mwingine kuwaingilia kinyume na maumbile watoto wao wa damu na wengine kuwaingilia watu wenye changamoto ya akili.
Amesema utandawazi ni sababu nyingine inayosababisha vitendo vya ukatili ambapo watoto wadogo wamekuwa wakipewa simu na wazazi wao,hivyo kuangalia vitu vilivyo kinyume na maadili na baadaye wanaenda kujaribu.
“Wazazi tumekuwa “bize”kutafuta maisha, kiasi kwamba mzazi anaondoka asubuhi anarudi jioni,kukaa na kuangalia watoto kwa karibu kitu hicho kimekuwa kigumu watoto wanajilea.Wengine vitendo vya ubakaji na ulawiti wanafundishana shuleni,” amesema Bilishanga.
Aidha ametaja sababu nyingine inayosababisha vitendo vya ukatili kuwa ni ulevi wa kupinduki, kwani wamekuwa wakipokea kesi nyingi za ubakaji maeneo ya kuuzia pombe, mfano wanawake walioolewa wanapolewa wamekuwa wakibakwa na mtu zaidi ya mmoja au mwanaume amelewa akifika nyumbani kwake anamwingilia mtoto wake au mfanyakazi.
Amebainisha kuwa waathirika wa vitendo vya ukatili kuwa ni wanawake na watoto wa miaka 12 hadi 16, kwani kuna watu wameishazisoma familia kwamba mama au baba akiondoka nyumbani anarudi muda fulani hivyo wanatumia mwanya huo kuwabaka watoto.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS),Mkoa wa Kagera, Wakili Seth Niyikiza,amesema makosa yalio kinyume na maadili ni pamoja na kujaribu kubaka, kumshikashika mtu bila ridhaa yake na kujinufaisha kingono kwa kushika viungo vyake.
“Kifungu cha 133 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16,kinaweka wazi kuwa mtu yeyote ambaye anamkamata na kumzuia mtu wa jinsia ya kike, ambaye ana umri wowote na kumfungia mahali fulani kwa nia ya kufanya naye mapenzi na mtu huyo alikuwa hajaridhia anafanya kitendo cha kupoka utu,” amesema Wakili Seth.
Ameitaka jamii kuwa na tabia ya kufuatilia sheria kujua zinahitaji nini au wawe na tabia ya kutekeleza sheria zilizowekwa
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba,Yona Wilson akizungumzia adhabu zinazotolewa kwa makosa ya ubakaji amesema kuwa, mwanaume aliyembaka au kumlawiti mtoto chini ya miaka 10 adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Amesema mwanaume ambaye amembaka au kulawiti mwanamke mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kwenda juu adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 na viboko.
Ameeleza kuwa, kwa upande wa kundi la watu ambalo limebaka au kuhusika kwa namna moja ama nyingine kubakwa kwa muhusika adhabu yao ni kifungo cha miaka 30.
“Kubaka kwa kundi siyo lazima mtu awe amemwingilia kimwili, kama mtu amesaidia kuhakikisha uharifu unatekelezwa basi hata huyo amehusika katika ubakaji huo hivyo naye anatuhumiwa kwa kosa hilo,” amesema Wilson.
Aidha, ametaja kosa jingine ni kupoka ambalo kifungo ni miaka saba, kumshikashika mtu bila ridhaa yake kwa ajili ya kujinufaisha kingono adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano.
More Stories
Serikali yaboresha sekta ya elimu Ulyankulu
Upungufu wa maji Mji Korogwe, HTM waeleza mikakati yao
Uwekezaji ufanyike maporomoko ya maji Kalambo