January 31, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mrindoko aweka kambi Njombe kujifunza kutomeza udumavu wa watoto

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Njombe.

MKOA wa Katavi na Njombe umeanzisha mkakati wa pamoja wa ushirikiano wa mapambano dhidi ya udumavu  ambao ni matokeo ya utapiamlo unaosababishwa na lishe duni na kujenga jamii yenye afya nzuri kwa maendeleo endelevu.

Ushirikiano huo ni matokeo ya agizo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alilotoa Julai 13, 2024 katika mkoa Katavi wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha wiki ya wazazi kitaifa,ambapo alimtaka mkuu wa mkoa Mwanamvua Mrindoko, kwenda kujifunza mkoa wa Njombe juu kukabiliana na udumavu ambao ni kikwazo kwa ustawi wa jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko Januari 30, 2025 ameweka wazi kuwa mwanzo wa ushirikiano wa mikoa hiyo miwili utasaidia kubadilishana uzoefu kwenye mambo mbalimbali ya kiafya, kiuchumi, kijamii na kiutalii.

Akiwa katika mkoa wa Njombe akitekeleza agizo la Rais Dkt Samia kwenda kujifunza namna bora ya kudhibiti udumavu, Mrindoko amesema ushirikiano huo ni mwanzo mzuri ambao unapaswa kusimamiwa.

“Tutaendelea kuwa marafiki wa kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya lishe na afya huku tukijikita zaidi pia kufanya tafiti za ndani ili kuonyesha hali halisi ya tatizo la udumavu” amesema.

Kiongozi huyo katika kuimarisha tafiti za ndani, amesema kuna jambo la lazima la kufanya kupitia wataalamu mbalimbali kuhakikisha wanafanya ili kuhuwisha takwimu za udumavu  kwani hadi sasa mkoa wa Katavi unatumia takwimu za mwaka 2022 zinazoonyesha asilimia 32.2 ya watoto chini ya miaka 5 wanaudumavu licha ya kwamba hapa katikati kunamabadiliko.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka, Licha ya kumpongeza Mrindoko kwa kutekeleza agizo la Rais Dkt.Samia amesema anaimani kubwa mkoa wa Katavi utafanya vizuri zaidi ya Njombe.

Mtaka ameeleza ushirikiano huo utajenga nguvu ya pamoja kukabiliana na udumavu na kuondoa rangi nyekundu kwenye takwimu za mikoa hiyo miwili.

“Tukiweka mashirikiano ya kiuchumi tutafanya vizuri lakini kunaeneo la elimu tunaweza tukashirikiana kwa maafisa elimu kuweka mitihani ya mashirikiano ya mikoa miwili kwa mitihani darasa la 7 kidato cha pili na nne hata cha sita” Amesema.

Amebainisha mbali na masuala ya lishe pia wanaweza kuchukua madaktari wa Katavi na Njombe na kufanya kambi maalumu kama jinsi wanavyofanya Wachina na watu wakafanya kliniki ya matibabu na kuwa daraja zuri la kushirikiana.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Katibu tawala, Wakuu wa wilaya za Tanganyika, Mpanda na Mlele na wataalamu mbalimbali wa mkoa huo wamekita kambi maalumu katika mkoa wa Njombe kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kudhibiti udumavu wa watoto ambapo mkoa wa Njombe ulitajwa na Rais Dkt Samia kufanya vizuri zaidi kutokomeza tatizo hilo la kiafya.