Na Mwandishi Wetu, Timesmajira
KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kwa Mkoa wa Kilimanjaro imezinduliwa huku suala la ardhi na ukatili wa kijinsia likitajwa kushamiri kwa migogoro na kuhitaji msaada wa kisheria.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema, kipaumbele kikuu kwenye kampeni hiyo mkoani humo ni utoaji wa elimu ya kisheria na hakuna jiwe ambalo halitaguswa kwenye migogoro sugu.
Akizindua jana Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) mkoani humo, Dk. Ndumbaro amesema watu wote watakaobainika kukiuka sheria, haki za binadamu, wanaonyang’anya watu haki za mirathi, wanaosababisha migogoro ya ardhi pamoja na wanaoendeleza ukatili wa kijinsia watachukuliwa hatua kali.
“Katika kampeni hii Tumekuwa tukianisha migogoro sugu ambayo haiishi ndani ya siku tisa za kampeni na kwa kushirikiana na TLS na wadau wengine tutarudi tena kushughulika na migogoro hiyo sugu, tunapiga gusa achia twende na Mama Samia, Tunaondoka na Ubaya Ubwela ili kila kitu kifanikiwe,”amesema.
Aidha, Dk.Ndumbaro amesema kuwa ni matokeo ya maono aliyokuwa nayo Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kubaini ya kuwa watu wengi wana kiu ya haki, jambo ambalo linadhibitishwa na umati mkubwa wa watu wanaojitokeza kwenda kupata ushauri wa kisheria kila mahali kampeni hiyo inapofanyika hapa nchini.
Ameeleza kampeni hiyo inasadifu falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Samia ambayo imeleta mabadiliko mengi na chanya hapa nchini kwa kuendeleza Amani.
“Amani imeendelea kutamalaki na hata kampeni hii ya msaada wa kisheria ni matokeo ya falsafa hii; kampeni hii imeleta faraja kwa Watanzania wengi haswa wale ambao walikuwa hawawezi kumudu gharama za kukodi wanasheria kwa ajili ya kushughulikia changamoto za kisheria walizonazo”, amesema.
Amewapongeza wale wote ambao wamejitokeza kupata huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo jambo ambalo alisema limedhihirisha ustaarabu wa watanzania wa kutafuta haki kupitia ngazi za kisheria badala ya kuitafuta kupitia maandamano kama ilivyo kwenye maeneo mengine duniani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema “Tutakwenda kwenye hadi vitongoji, ni kweli Mkoa wa Kilimanjaro lipo tatizo kubwa la ardhi kwasababu ardhi ni finyu na ilishagawanywa kwa muda mrefu na waliokuwa nayo, watu wanaongezeka na wanaendelea kuzaliana.”
Pia, amesema suala la ukatili upo mkubwa na Mkoa umekuwa ukichukua hatua kupunguza hali hiyo na kwamba watu 30 wamehukumiwa kifungo jela kwa ubakaji na ulawiti na kutoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya kampeni hiyo ili kupata msaada wa kisheria.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati hususan kwa wananchi wanyonge.
Amesema kampeni hiyo itafanyika mkoani humo kwa siku tisa mfululizo kuanzia Vijiji, Mitaa, Kata na kuzunguka kwenye Halmashauri zote saba.
Amesema watatoa elimu kuhusu masuala ya kisheria, utawala bora, mapambano ya ukatili wa kijinsia, Haki za binadamu, masuala ya ndoa, usimamizi wa mirathi, haki za ardhi kwa kuwa Kilimanjaro ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili.
“Tutatoa ushauri wa kisaikolojia kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia, huduma za msaada wa kisheria kwenye sehemu za vizuizi kama Magerezani, vituo vya polisi na maeneo yenye mikusanyiko sokoni, minadani, shule na vyuo na kupitia kampeni hii viongozi wa serikali za mitaa, mabaraza ya kata, ardhi na ndoa yatajengewa uwezo katika masuala ya kisheria,”
Pia alisema kampeni hiyo itahusisha elimu ya Katiba na uraia kwa viongozi mbalimbali ikiwamo kamati ya usalama ya Mkoa na Wilaya zake.
“Tangu kampeni izinduliwe Aprili 2023, Mikoa 17 imefikiwa ambayo ni Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Singida, Njombe, Iringa, Mara, Songwe, Morogoro, Kigoma, Katavi, Mtwara, Tabora, Geita na Kilimanjaro,”amesema.
Amesema lengo ni kuhakikisha mikoa yote nchini inafikiwa na wananchi wa pembezoni wanapata haki kwa wakati.
Naye, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, alisema huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa kupitia kampeni hiyo ni ibada kwa kuwa ni suala linaloshughulika na maisha ya watu.
Amehimiza wananchi umuhimu wa kuandika wosia kwa kuwa ni moja ya njia nzuri zinazosaidia familia zisinyang’anywe mali pindi baba au mama anapofariki.
Mmoja wa wakilishi wa watoa huduma za msaada wa kisheria, Wakili Elizabeth Minde amesema maeneo yenye kadhia kubwa kwenye masuala ya kisheria ni migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia na mirathi.
“Hata kesi zinazokwenda mahakamani zinazohusu mirathi zinaleta mgongano mkubwa na inatokana na hata hizo sheria za mirathi zipo nyingi na haijulikani watu wafuate utaratibu gani, kupitia kampeni hii tunaomba kwa heshima suala la sheria ya mirathi liangaliwe na irekebishwe ili isaidie wananchi kuwa na amani na utulivu,”amesema.
WANANCHI WAFUNGUKA
Mkazi wa Manispaa ya Moshi, Jackline Tibamanya, amesema mume wake alifariki mwaka 2021 hadi leo bado yupo kwenye kesi ya mirathi ameanza kupambana tangu Mahakama ya mwanzo mkoani Kagera na sasa yupo Mahakama Kuu na yeye ndio msimamizi mkuu wa mirathi lakini kimada wa aliyekuwa mume wake ameng’anyania nyumba.
Ameomba suala hilo lishughulikiwe ili watoto wake wapate mahali pa kuishi kwa kuwa huyo kimada amegushi nyaraka.
Mkazi wa Moshi, Grace Mushi alisema ametelekezewa watoto watano na Baba wa watoto hawatunzi kwa mahitaji yeyote kwa kipindi cha miaka sita hivi sasa.
Mwingine, Claudia Shirima amesema ardhi yao imevamiwa na kesi inaendelea kwenye baraza lakini hadi sasa hakuna lililoamuriwa.
Kutokana na hoja hizo, Dk. Ndumbaro amesema katika kampeni hiyo wananchi wote wenye changamoto watasikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi.
More Stories
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele
TARURA Kilindi kutumia bil.5.2 bajeti 2025/26
Madiwani Kilindi wapitisha bil.36.8 bajeti 2025/26