Na Penina Malundo,Timesmajira
MARAIS na viongozi wakuu wa nchi za Afrika wamepitisha na kusaini Azimio la Dar es Salaam (M300) linalohusu masuala ya nishati, likilenga kuhakikisha umeme na nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu kwa wananchi wa Afrika.
Katika Azimio hilo, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo shindanishi ya manunuzi ya umeme, kuvutia wazabuni wenye uwezo, na kuleta usawazisho katika sekta ya fedha kwa kuimarisha mifumo na mipango ya bei, viwango na kushirikiana zaidi miongoni mwa nchi ili kunufaika na fursa zilizopo za umeme.
Akisoma azimio hilo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Profesa Vincent Nmehielle, alisema kuwa Azimio la Dar es Salaam limepitishwa na kusainiwa na Marais na Wakuu wa Nchi za Afrika katika mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika, ulioanza juzi, Januari 27, 2025.
Profesa Nmehielle alisema kuwa viongozi hao wamekubaliana kuwa ili kufikia lengo la saba la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) la Umoja wa Mataifa, ambalo linahusisha upatikanaji wa nishati kwa wote ifikapo 2030, ni lazima kuwepo na lengo la pamoja katika mnyororo mzima wa nishati barani Afrika.
“Miongoni mwa vipengele muhimu vilivyomo katika Azimio hilo ni pamoja na kupitisha mkataba wa pamoja wa nishati kwa ajili ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya nishati hadi mwaka 2030. Marais na Wakuu wa Nchi wametambua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, na kuongeza jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kufanikisha agenda ya nishati, inayojulikana kama ‘Agenda 300’,” amesema prof . Nmehielle.
Ameongeza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia zimejizatiti kuhakikisha kuwa watu milioni 250 wanapata umeme na nishati safi ya kupikia kupitia mradi huo, na wameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kutenga fedha na kufadhili miradi hiyo hadi mwaka 2030.
“Kupitia Azimio hili, tunalenga kuvutia zaidi mitaji ya sekta binafsi ili kuhakikisha fedha zinazohitajika kwa ajili ya mabadiliko ya mifumo ya nishati Afrika zinapatikana na kutekelezwa kwa ufanisi,” amesema Prof. Nmehielle.
Kipengele kingine muhimu kilichozungumziwa ni kuhusu ahadi za Benki ya Maendeleo ya Afrika kutenga dola bilioni 2.6 kwa ajili ya miradi ya upatikanaji wa umeme barani Afrika.
Viongozi walikubaliana kutambua mchango wa wadau wa kifedha na ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huu wa maendeleo ya nishati.
“Pia, viongozi hao walikubaliana kutambua jitihada za Afrika katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na utengamano wa kikanda, na kuhakikisha kuwa Umoja wa Afrika unatekeleza majukumu yake kimkakati kwa ajili ya soko la pamoja la nishati,” alisema prof Nmehielle.
Nmehielle alisisitiza pia umuhimu wa sekta binafsi katika mnyororo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa nishati safi, na kusema kuwa mazingira wezeshi yataendelea kubuniwa kwa sekta binafsi ili kutoa mchango mkubwa katika kufikia malengo ya nishati.
Kipengele kingine kilichojadiliwa ni kuhusu kuhakikisha miundombinu ya umeme inapatikana kwa gharama nafuu na endelevu.
Viongozi wamekubaliana kupitia hatua mbalimbali ikiwemo kurekebisha gharama za umeme na kuhakikisha huduma za umeme zinapatikana kwa gharama ndogo na kwa muda muafaka.
“Azimio hili linatoa msukumo mkubwa kwa sekta binafsi kujikita katika kuanzisha mifumo ya ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa umeme, na kuhakikisha kuwa nishati safi ya kupikia inawafikia watu wengi, hususan wanawake na watoto,” amesema.
Viongozi pia wamekubaliana kuhakikisha upatikanaji wa fursa katika sekta ya nishati na kutengeneza ujasiriamali, huku wakizingatia masuala ya usawa wa kijinsia, ili kuhakikisha kuwa wanawake wanapata nishati safi na inayokidhi mahitaji yao.
“Tutahakikisha kuwa fursa za ujasiriamali zinapatikana kwa vijana, na Serikali za Afrika zitashirikiana na wadau wa kimataifa katika kutekeleza mipango ya nishati, huku tukizingatia pia kutenga bajeti za kitaifa kwa ajili ya miradi ya nishati,” amesisitiza Prof. Nmehielle.
Azimio la Dar es Salaam limepitishwa na Marais na Wakuu wa Nchi za Afrika, na litakuwa mwongozo muhimu katika kuhakikisha Afrika inafikia malengo yake ya upatikanaji wa nishati kwa wote ifikapo 2030
More Stories
Ilemela yakusanya bilioni 7, mapato ya ndani
Madiwani Ilemela wapitisha rasimu ya bajeti bilioni 84.3
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele