Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.
MKUU mpya wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega,ameapishwa rasmi leo, Januari 29, 2025 katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Songwe, zilizopo eneo la Selewa.
Mbega, aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Januari 24, 2025, anachukua nafasi ya marehemu Ester Mahawe, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Akitoa neno la shukrani baada ya kuapishwa, Mbega alimshukuru Rais kwa kumuamini na kumpatia nafasi ya kuongoza wilaya hiyo.
Pia, aliahidi kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika Wilaya ya Mbozi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Songwe, alimpokea rasmi Mbega na kumuahidi ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika hafla hiyo, alimtaka Mbega kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, uaminifu, na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, akizungumza baada ya kumaliza jukumu la kumuapisha, alimpongeza Mbega kwa uteuzi wake na kumtaka kutumia ujuzi wake kuhakikisha Wilaya ya Mbozi inapiga hatua za maendeleo.
Chongolo alitumia fursa hiyo, kumpatia majukumu mahususi ya kuanzia kwa Mkuu huyo mpya, ambayo ni kudumisha amani na utulivu, huku akimtaka kutilia mkazo masuala muhimu kama vile mimba za utotoni, mdondoko kwa wanafunzi shuleni, ikiwemo, suala la suala la udumavu kwani licha ya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wazalishaji wa chakula, lakini bado viwango vya udumavu viko juu.
Aidha, Chongolo alimtaka Mbega kuchukua hatua madhubuti dhidi ya uhalifu, hususan vitendo vya ulawiti na ubakaji, pamoja na kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa maendeleo endelevu ya wilaya hiyo.
More Stories
TAKUKURU yabaini miradi nane yenye dosari
Ilemela yakusanya bilioni 7, mapato ya ndani
Madiwani Ilemela wapitisha rasimu ya bajeti bilioni 84.3