Na Mwandishi Wetu
MKUTANO wa Nishti barani Afrika ambao umefanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam umevunja rekodi kwa kuhudhuriwa ma marais wengi kwa wakati mmoja.
Rekodi hiyo imeandikwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo. Mkutano huo ulianza juzi Januari 27 na kuhitimishwa jana.
Mkutano huo umehudhuriwa na marais 21 wa nchi za Afrika ambao walikutana na kujadili mustakabali wa nishati katika bara Afrika.
Marais hao 21 ni kati ya 25 waliothibitisha kushiriki na wengine wamewakilishwa na viongozi wengine wa juu wa Serikali zao.
Marais hao 21 waliohudhuria waliongozwa na mwenyeji wap, Rais Samia.
Marais wengine ni wa Lesotho, Djibouti, Jamhuri ya Congo Brazzaville, Visiwa vya Comoro, Madagascar, Somalia, Sierra Liane na Mauritania.
Wengine ni kutoka Burundi, Guinea Bissau, Malawi, Libya, Zambia, Kenya, Nigeria, Gabon, Liberia, Ethiopia, Botswana na Ghana.
Marais hao wanaifanya Tanzania kuandika rekodi mpya, kwani haijawahi kushuhudiwa marais wengi kiasi hicho kuhudhuria mkutano huo.
Kabla ya rekodi hiyo ya marais wengi kukutana nchini kwa wakati mmoja ilikuwa mazishi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1999, yaliyohudhuriwa na wakuu wa nchi 19.
Pia, tukio la pili lilikuwa Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa mwaka 2019 ulioshirikisha wakuu wa nchi 15, lakini safari hii idadi imepaa hadi 21.
Wakuu hao wa mataifa 21, walikuwa na jukumu la kuazimia kile kilichojadiliwa na mawaziri wa kisekta katika mkutano huo juzi kadhalika walitakiwa kuahidi mabadiliko ya sera na sheria kurahisisha uwekezaji wa sekta binafsi katika nishati.
Sambamba na hayo, walishuhudia utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa Ajenda300 inayolenga kuhakikisha mwaka 2030, Waafrika milioni 300 watafikiwa na huduma ya umeme.
Mkutano wa wakuu hao ulitazamiwa kutoka na kauli moja kuhusu mustakabali wa upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wakazi wa Afrika ambao milioni 600 wapo gizani.
Chimbuko la mkutano huo ni maazimio ya Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zilizokubaliana kuhakikisha mataifa ya Afrika yanaondokana na giza.
Hata hivyo, hatua ya kuanza na nchi 14 ni mwanzo tu, lakini kadri siku zinavyokwenda idadi ya nchi zinatarajiwa kuongezwa, hadi umaskini wa nishati utakapokoma barani humo. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo
Tanzania inazalisha zaidi ya Megawati 3,000 za nishati hiyo, huku mahitaji ni 1,800 ingawa ni asilimia 78 tu ya wananchi ndiyo wanaopata huduma hiyo kwa sasa.
Juhudi zinazohitajika ni kutengeneza uwiano kati ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini na Afrika, hilo ndilo linalojadiliwa na wakuu hao wa nchi na watatoka na kauli moja.
More Stories
Manispaa ya Shinyanga yaandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza kwa 99%
TAKUKURU yabaini miradi nane yenye dosari
Ilemela yakusanya bilioni 7, mapato ya ndani