Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali amezuia Waalimu kulima mashamba ya shule kwa matumizi yao binafsi,huku akitaka yatumike kwa ajili ya shule,ili waweze kupata mahindi yatakayowezesha wanafunzi kupata chakula shuleni.
Juakali amesema hayo,Januari 28,2025, katika ziara alioifanya ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, baada ya kumtembelea shule ya sekondari Chala,ambapo alikuta imelima hekali mbili tu,wakati shule hiyo inazo hekali 180 ambazo walimu wamegawana huku maeneo mengine wakiyakodisha kwa wananchi.
Amesema kuwa Wilaya hiyo kwa sasa ina mpango madhubuti wa kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni.Mkakati uliopo ni maeneo ya ardhi yanayomilikiwa na shule, yanatumika kuzalisha chakula cha kutosha na kuondoa usumbufu kwa wazazi wa kuchangia chakula shuleni wakati shule zenyewe zinazo uwezo wa kuzalisha chakula.
Hivyo,walimu wote wa shule za msingi na sekondari wilayani Nkasi,hawapaswi kugawana mashamba ya shule wala kukodisha kwa wananchi,hadi wapate kibali kutoka kwake.
Huku akiagiza shule zote ambazo Walimu wamelima mashamba ya shule,apate orodha yao ofisini kwake mara moja kwa ajili ya maamuzi mengine zaidi.
Amesma,shule nyingi wilayani Nkasi zina maeneo makubwa kwa ajili ya kilimo,hivyo rasilimali hiyo ikitumika vizuri, itasaidia kupatikana chakula shuleni kwa mwaka mzima bila ya wazazi kuchangia chochote.
Pamoja na hayo,amewataka Watendaji wa Serikali kuwa waadilifu kwenye usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekekezwa katika maeneo yao,ili iwe na tija kwa Wananchi.Huku Wilaya kwa sasa imetekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 6.
Miradi hiyo aliyoitembelea Jana ni ujenzi wa Mabweni ya Wavulana shule ya sekondari Nkasi,madarasa shule ya msingi Kipundukala, shule mpya ya sekondari Majengo,shule mpya ya sekondari Isunta,Madarasa ya kidato cha Tano na Sita shule ya sekondari Ntatumbila,shule mpya ya msingi Chala,ujenzi wa Madarasa shule ya sekondari Chala,ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Londokazi.
More Stories
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele
TARURA Kilindi kutumia bil.5.2 bajeti 2025/26
Madiwani Kilindi wapitisha bil.36.8 bajeti 2025/26