January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA :Mvua za masika kuanza mwanzoni mwa mwezi Machi

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi Utabiri wa Msimu wa Mvua za Masika 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ambapo zinatarajiwa kuanza wiki ya Pili au ya tatu ya mwezi machi mwaka huu.

Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu huku mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zikitarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria.

Amesema Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Mashariki mwa Mikoa ya Mara na Simiyu.

Amesema mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara) katika kipindi cha Msimu wa Masika, 2025.

Vilevile,amesema ongezeko la mvua hizo zinatarajiwa katika kipindi cha mwezi Aprili sambamba na kutoa angalizo la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo zinaweza kupelekea upungufu wa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji.

Dkt.Changa alisema katika msimu huo wa mvua za masika zinatarajiwa kuwa na ongezeko la mvua kwa mwezi Aprili, 2025.
”Utabiri wa Msimu wa Mvua za Masika 2025 kwa maeneo ni mahsusi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

”Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mkoa wa Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia),Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara),”amesema.

Aidha amesema Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.

Akizungumzia athari zinazotarajiwa kutokea ni pamoja na Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani,Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka na Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.

Amesema kupitia mkutano wa wadau wa hali ya hewa uliofanyika Januari 20 2025, na pia mkutano na Wanahabari uliofanyika Januari 22,2025,wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii wanashauriwa kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

”Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani, wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea yanayoendana na hali ya ongezeko la unyevu kama vile ukungu yanatarajiwa kuongezeka na kuathiri mazao kama ndizi, mahindi,mpunga, mihogo na maharage,”amesema.

Amewashauri wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, kuhifadhi maji shambani, kuzuia mmomonyoko na upotevu wa rutuba kutokana na kutuwamisha maji kwa muda mrefu au mafuriko.

”Wakulima wanashauriwa kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa msimu wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi.”amesisitiza.

Pia amesema wakulima na maafisa ugani wanashauriwa kuendelea kutumia utabiri wa siku na siku kumi ili kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa utabiri wa msimu.