Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraonlineTabora
WAKAZI wa Mkoa wa Tabora wakiongozwa na wazee, viongozi wa dini, viongozi wa chama na serikali na mamia ya wananchi wameandamana kumpongeza Dkt Samia Suluhu Hassan, Dkt Hussein Mwinyi na Dkt Emanuel Nchimbi kwa kupitishwa kuwa wagombea Urais mwaka huu kupitia CCM.
Wakizungumza kwenye maandamano hayo ya amani yaliyofanyika jana kuanzia Ofisi ya CCM Mkoa hadi viwanja vya CCM Wilaya ya Tabora Mjini, walisema wamefurahishwa na uamuzi wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jijini Dodoma.
Mzee Seif Mohamed mkazi wa Mwinyi katika manispaa hiyo, alisema wameandamana ili kuunga mkono mapendekezo hayo kwa kuwa viongozi hao wameonesha uwezo mkubwa katika uongozi wao.
‘Tumefurahishwa sana na uamuzi wa kupitishwa Rais Samia, Rais Mwinyi na Katibu Mkuu wa CCM Dkt Emanuel Nchimbi kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa Rais, Wabunge na Madiwani’, alisema.
Mwanachama wa UWT Mkoani hapa Hadija Mohamed alieleza kuwa kasi ya maendeleo yaliyoletwa na Rais Samia na Rais Mwinyi kwa Zanzibar ni kielelezo tosha kuwa viongozi hawa wanatosha kupewa mitano tena.
‘Rais Samia ni mwanamke shujaa na kiongozi makini mwenye maono makubwa ya kimaendeleo, tumepokea uteuzi huo kwa mikono miwili, akinamama wa Mkoa wa Tabora tunaunga mkono mapendekezo hayo kwa asilimia 100,” alisema.
Askofu Elias Mbagata wa Kanisa la Injili Afrika la Mjini hapa, alisema Rais Samia, Rais Mwinyi na Emanuel Nchimbi ni chaguo sahihi, wana kila sifa zinazotakiwa na watanzania wameonesha uwezo mkubwa kiutendaji.
‘Watanzania wana kila sababu ya kuwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa maamuzi hayo ambayo yatawapa nafasi wagombea hao wa CCM kujipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaohusisha vyama vya upinzani’, alisema.
Mchungaji Shedrack Augustino wa kanisa la KCC alisema CCM imeonesha ukomavu wa hali ya juu na kuwa mfano wa kuigwa na vyama vingine kwa kufanya maamuzi yenye maslahi kwa chama na taifa kwa ujumla.
Akitoa salamu za chama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Said Nkumba, alisema CCM itaendelea kuchagua viongozi makini, wazalendo, wachapa kazi, wanaojali watu na siyo maslahi binafsi na wenye kauli safi.
Alisema kuwa Rais Samia na Rais Mwinyi wamethibitisha kwa vitendo weledi wao ndiyo maana wajumbe wakafanya maamuzi hayo, CCM ndicho chama pekee kinachoruhusu wagombea wake kupimwa na wanachama tangu ngazi ya chini ili kupanua demokrasia.
‘CCM imefanya maamuzi yake mapema ili kila mtu ajue watakaogombea nafasi hizo, sisi sio kama vyama vingine ambavyo wagombea wao wanatambulishwa dakika za jioni tena kwa kushitukiza wapiga kura, hakuna haja ya kuficha,” alisema.
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru