January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi

Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi.

Na George M wigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

SERIKALI inaendelea kutekeleza  mkakati mpya wa kampeni ya kitaifa wa utoaji wa  msaada wa kisheria kwa wananchi wa mkoa wa Katavi ili kujega uwezo kwa wananchi kutambua haki zao na kukabiliana na matatizo ya kisheria.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanavua Mrindoko, Januari 22, 2025 akizungumza na wanahabari ambapo amesema kampeni hiyo  itatekelezwa kwa mara ya kwanza mkoani humo Januari 24 mwaka huu na kudumu kwa muda wa siku kumi.

Amesema huduma hiyo ya msaada wa kisheria ambayo inatekelezwa bila malipo ya fedha kwa wananchi itasambazwa kuanzia maeneo ya mjini hadi vijijini ambako kumeshuhudiwa mizozo ya ukosefu wa haki kwa sababu ya uelewa mdogo wa mambo ya kisheria.

Akiwa ofisini kwake, Mrindoko ameeleza kampeni hiyo inayoitwa Mama Samia Legal Aid itafanyika katika halmashauri ya Nsimbo,Tanganyika, Mlele, Mpimbwe, Mlele na manispaa ya Mpanda ambapo italinda, kukuza na kutetea haki za wananchi wanyonge na kupinga vitendo vya uvunjifu vya haki za binadamu.

Kiongozi huyo ameweka wazi licha ya kampeni hiyo kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria pia itasaidia kutatua matatizo ya kisheria ambayo wananchi hawajapata ufumbuzi wa haki zao za kisheria.

Mrindoko amesema “ kampeni hii yenye kauli mbiu inayosema msaada wa washeria kwa haki sawa, amani na maendeleo ni dhahili inaashiria adhima ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuelewesha umma  kuhusu misingi ya utawala bora”

Kampeni hiyo vilevile itaimarisha juhudi za  kupinga vitendo vya ukatili vya kijisia, kuendelea kuhamasisha wananchi kuheshimu utawala bora na utawala wa sheria ambapo vyote ni msingi wa maendeleo.

Katika kuhakikisha wananchi  wanashiriki kampeni hiyo, ameomba wananchi kujitokeza  kwenye uzinduzi utakao fanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kashauriri manispaa ya Mpanda na maeneo mengine ya mkoa huo ili kupata fursa ya matatizo yao kushughurikiwa hapo kwa hapo na yale ambayo hayatapatiwa ufumbuzi yatachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa haraka kupitia wizara ya Katiba na Sheria.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) itaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinafia Watanzania kwa ufanisi huku wengi wakiamini kampeni hiyo pia inafanyika kwa njia ya mtandao sasa wananchi watapatiwa nyenzo zitakazo wawezesha kuzifikia haki zao.