November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wenye madeni ya Umeme wapewa siku 14

Na Mwandishi wetu, TimesMajira, Online

WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa siku 14 kwa wateja wote wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wenye malimbikizo ya bili za Umeme kuhakikisha wanalipa madeni yao ama kusitishiwa huduma baada ya muda huo kupita.

Waziri Kalemani ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Miradi na kazi mbalimbali za Umeme Jijini Arusha.

Amesema, hadi sasa wanadai bilioni 69.7 kwa watu binafsi na bilioni 307 kwa Taasisi za Umma hivyo anawasihi watu wenye malimbikizo ya madeni hayo kulipa fedha ndani ya siku hizo.

“Hatutaki kupokea simu kulalamika, tunataka kupokea malipo, tusisahau kuwa TANESCO ni Shirika la kibiashara ambalo linajiendesha kwa mapato yake bila kutegemea ruzuku ya Serikali hivyo kuchelewesha malipo ya Ankara za Umeme ni kuchelewesha juhudi za Shirika hili kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi kwa huduma bora na za Nishati ya umeme ya uhakika,”amesema Waziri Kalemani

Pia amewasisitiza wateja wote wakiwemo binafsi na Taasisi za Kiserekali kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati kwani muda wa kusitisha huduma kwa wasiolipa ukifika, TANESCO na Wizara hawatasikiliza wala kupokea simu za maelezo ya mdaiwa sugu yeyote yule isipokuwa kusitisha huduma ya Umeme mpaka deni litakapolipwa