Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
MWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa maamuzi yake ya busara ya kumchagua kwa kura nyingi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025.
Mgeja ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, ametoa pongezi hizo kufuatia wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kumchagua mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu.
Mbali ya kuchaguliwa kwa Dkt. Samia lakini pia mkutano huo ulimchagua Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar huku Dkt. Emmanuel Nchimbi akitangazwa rasmi kuwa mgombea mwenza wa Dkt Samia Suluhu Hassan.
Mgeja amesema maamuzi ya wajumbe wa mkutano mkuu yameonesha jinsi gani CCM ilivyokomaa kidemokrasia na kwamba yeye binafsi anatoa pongezi nyingi kwa wana CCM na viongozi wote wakuu ndani ya CCM kwa kufanya jambo kubwa la busara.
“Maamuzi haya ya wajumbe yameonesha imani kubwa kwa mwenyekiti wetu wa CCM Taifa kwamba kazi kubwa anazozifanya watanzania ni kubwa na matokeo yanaonekana na wananchi wanaziona, hivyo ushindi huu wa asilimia 100 ni ushindi unaodhihirisha kuwa wana CCM na wananchi kwa ujumla bado wana imani na Rais Samia,”
“Binafsi nina imani kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kitafanya vizuri na wagombea wake wote watashinda uchaguzi huo kwa kishindo, na niendelee kumpa hongera Rais Samia na Dkt. Hussein Mwinyi, nasema 2025 kwa kazi hizi zinazotekelezwa na viongozi hawa, 2025 ushindi ni lazima,” ameeleza Mgeja.
Ameendelea kueleza kuwa hata kwa upande wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi amefanya kazi kubwa, maendeleo ambayo yamepatikana ndani ya kipindi cha miaka minne yanaonekana na kwamba mapinduzi kwa upande wa maendeleo kwenye visiwa hivyo yanakwenda kwa kasi kubwa.
Kuhusu uteuzi wa Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu ujao, Mgeja amesema ni uteuzi wa busara na mtu ambaye ameteuliwa ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo ya Umakamu wa Rais.
“Lakini pongezi za pekee pia zimwendee Dkt. Emmanuel Nchimbi (balozi) ambaye pia ni Katibu Mkuu wetu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa uteuzi wa kuwa mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi, hii ni imani kubwa kwa Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa,”
“Pia ni imani kubwa kwa Chama cha Mapinduzi lakini na kwa Dkt. Nchimbi mwenyewe kwa vile uteuzi huu umeonesha jinsi gani CCM inavyothamini utendaji wake ndani ya Chama na hivyo wameona ni vyema sasa asimame kwenye nafasi hiyo ya ugombea wenza, tunampongeza,” ameeleza.
Amesema Dkt. Nchimbi amelelewa na kukulia ndani ya Chama, anakijua vizuri chama, lakini pia amewahi kufanya kazi katika sehemu mbalimbali ndani ya Serikali, kuanzia ukuu wa wilaya na balozi, hivyo naamini anaifahamu vyema Serikali na hivyo ana uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya kidiplomasia.
Kutokana hali hiyo Mgeja amekipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kumpata mgombea mwenza ambaye ni sahihi na kwamba anaamini Dkt. Nchimbi atafanya kazi zake vizuri hasa ikizingatiwa kuwa bado ni kijana na damu yake inachemka.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao