Na Allan Kitwe, Timesmajiraonline Tabora
WADAU, wanaCCM na baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani Mkoani Tabora wamepongeza uamuzi wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kuwapitisha Rais Samia na Rais Mwinyi kuwa wagombea wa Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wametoa pongezi hizo jana walipokuwa wakiongea na mwandishi wa gazeti hili mara tu baada ya kupitishwa Azimio hilo ambalo limeungwa mkono na wajumbe wote kwa asilimia 100.
Walisema kuwa uamuzi huu umeonesha jinsi wana CCM walivyokomaa kisiasa na wanavyotanguliza mbele maslahi ya wananchi tofauti na vyama vingine vya kisiasa hapa duniani.
Mwanaharakati mkazi wa halmashauri ya manispaa ya Tabora Elisha Daudi alisema kuwa uamuzi huo unawapa ari, nguvu na motisha ya kufanya mambo makubwa zaidi ya yale waliyoyafanya ili kuwanufaisha wananchi.
Alieleza kuwa muda wa kuteua wagombea ulikuwa haujafika, lakini weledi, uzalendo na ufanisi mkubwa uliooneshwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na mwenzake Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi umewagusa sana wajumbe.
‘Uamuzi huu unasaidia sana kupunguza vurugu za kisiasa ndani ya chama na wale wanachama vihele hele wasio na hekima ndani ya chama wanazibwa midomo mapema, hivyo wajumbe wamefanya uamuzi sahihi na kwa wakati’, alisema.
Mkazi wa Ipuli na mwanachama wa CCM Elias Kayandabila alieleza kufurahishwa na uamuzi huo kwa kuwa unawapa nafasi wagombea kujipanga vizuri zaidi na kuepusha makundi yasiyo na tija.
‘Rais Samia na Rais Mwinyi ni wachapa kazi wazuri na ni viongozi makini wasio na makuu katika utendaji wao, ndio maana wajumbe wa Mkutano huo Mkuu wameamua kuwapitisha moja kwa moja pasipo kupepesa macho’, alisema.
Alibainisha kuwa licha ya Katiba ya CCM kuwapa nafasi nyingine ya kuingia kwenye kinyanganyiro cha kuwania nafasi hiyo dhidi ya wagombea wengine wa vyama vya upinzani, wajumbe wametumia busara ili kuepusha mvurugano.
Hamis Lusajo, mwanachama wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoani hapa alipongeza wajumbe hao kwa kufanya maamuzi yenye busara mapema kabla ya wanaCCM wenye mihemko hawajaanza kukivuruga chama hicho.
Alifafanua kuwa Kiongozi mzuri anaonekana mapema, apewe nafasi, tatizo ni wanasiasa wenye tamaa, hao ndio wanaoingiza vyama kwenye vurugu, misuguano na kuanzisha makundi, tunawapongeza sana wana CCM.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro