January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apongezwa kuwezesha ujenzi ofisi kuu WMA

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) jijini Dodoma akisema ni matumizi mazuri ya fedha za Watanzania.

Aliyasema hayo jana 2025 baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo hilo ambalo limegharimu sh. bilioni 6.2 na liko katika hatua za mwisho kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Dkt. Abdallah alisema kuwa lengo la ujenzi wa jengo hilo ni kuhakikisha utoaji huduma katika sekta ya biashara hususan katika bidhaa zinazotoka viwandani unaboreshwa.

Akifafanua, alisema kuwa maboresho ya kutoa huduma bora katika sekta ya biashara na katika uendelezaji wa viwanda ni pamoja na kuwa na mazingira mazuri kwa wafanyakazi na yale ya utoaji wa huduma hizo.

“Na katika hili, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi makubwa, mojawapo ikiwa ni ujenzi wa jengo hili ambalo tunakwenda kulizindua hivi karibuni,” alisisitiza.

“Ninyi wenyewe ni mashahidi; fedha za Watanzania zinaenda kukamilisha ujenzi huu ili tuweze kutoa huduma bora katika jamii ya wafanyabiashara ili tuweze kuleta maendeleo na tija katika sekta ya viwanda,” aliongeza Katibu Mkuu.

Kuhusu mtazamo wake kutokana na maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, Katibu Mkuu Hashil alieleza kuwa kwa mujibu wa maelezo na uthibitisho uliotolewa pamoja na kujionea kwa macho kazi inavyoendelea, ni dhahiri Mkandarasi atakamilisha kazi ndani ya muda ulioafikiwa ambao ni Februari 10 mwaka huu.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, pamoja na kuunga mkono pongezi na shukrani kwa Rais Samia kuwezesha ujenzi wa jengo hilo, pia amebainisha kuwa ujenzi umefikia asilimia 95.2 na kwamba kukamilika kwake siyo tu kutaboresha mazingira ya wafanyakazi wa Wakala bali pia kwa Serikali kwa ujumla.

Akidadavua baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na kukamilika kwa jengo hilo, Mtendaji Mkuu alieleza kuwa maabara ya kisasa ndani yake itawezesha kuhifadhi vifaa ambavyo kitaalamu vinajulikana kama vyenye usahihi wa kati au kwa lugha ya kigeni ‘secondary standards’

“Niwakumbushe tu kuwa, Wakala wa Vipimo ndiyo umepewa jukumu la kuhifadhi vipimo vyenye usahihi wa kati, kwa maana pale ndiyo tunalinganishwa kimataifa na ndipo unaleta ongezeko la Imani kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini wakijua kwamba usahihi wa vipimo unafuatiliwa kutoka ngazi ya mfanyabiashara mpaka ngazi ya kimataifa.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mwakilishi wa Mkandarasi anayejenga jengo hilo kutoka Kampuni ya Mohamed Builders, Bwana Burhan Hamza pamoja na Mshauri Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Bi Rachel Lista wamethibitisha kuwa jengo litakamilika na kukabidhiwa kwa WMA Februari 10, 2025.

Ujenzi wa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo, lililopo eneo la Medeli jijini Dodoma ulianza Julai 2, 2022 na matarajio ilikuwa likamilike Desemba 30, 2024 lakini Mkandarasi aliomba kuongezewa siku 40 kutokana na changamoto ndogondogo alizokutana nazo. Hadi sasa Mkandarasi amelipwa jumla ya sh.bilioni 5.8 kati ya shilingi bilioni 6.2 ambayo ni gharama ya utekelezaji wa Mradi huo.