January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ng’ombe 10 wamekufa kwa kupigwa na radi

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi


NGO’MBE 10 wamekufa papo hapo baada ya kupigwa na radi Januari 13,2025,kijiji cha Mwenge Kata ya Kate wilayani Nkasi wakiwa malishoni.


Akizungumzia tukio hilo Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kate, Deus Njugu,amesema kuwa ng’ombe hao walipigwa na radi jana majira ya saa 9 alasiri wakiwa malishoni.Wakati radi hiyo inapiga palikua na ng’ombe 15 na wote walindondoka chini lakini baada ya muda ng’ombe 5 walisimama na kuondoka huku 10 wakiwa wamekufa.


Amesema kati ya ng’ombe hao waliokufa madume 5 na majike 5,ambao ni mali ya Steven Slanda mkazi wa Kijiji hicho cha Mwenge.


Amefafanua kuwa ng’ombe hao baada ya kufa kwa radi walianza kujaa matumbo,huku kijana aliyekua akiwachunga akiwa salama.


Awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwenge,Charles Kafumu amekiri kutokea kwa tukio hilo,ambapo amesema matukio ya radi ambayo yamekua yakitokea mara kwa mara kijijini hapo na kusababisha madhara ikiwemo vifo,yamekuwa yakiwaweka njia panda na hawajui nini cha kufanya.


Amedai kuwa karibia kila mwaka inapofika msimu wa mvua za masika,lazima radi ipige na kusababisha madhara kwa jamii kama hayo ya mifugo kufa na hata binadamu au vyote kwa pamoja.


Ofisa Mifugo Kata ya Kate,Leticia Kahabi, amesema ng’ombe hao hawatakiwi kuliwa kwani wana madhara ya kiafya,hivyo inabidi wafukiwe na asiwepo mtu mwenye uwezo wa kuweza kuipata nyama hiyo na kuitumia kama kitoweo.


Amesema,kwa mujibu wa sheria na kanuni za kiafya hairuhusiwi kula nyama ya mnyama ambaye hajachinjwa,ambapo mnyama aliyekufa kwa kupigwa na radi nyama yake inakua na chembechembe ya umeme wa radi ambao ina madhara kwa mtu anayekwenda kuitumia nyama hiyo kama kitoweo.


Diwani wa Kata ya Kate,Dismas Msangawale amewataka wakazi wa Kate kuwa watulivu katika kipindi hicho linapotokea tukio la namna hiyo na kuacha kuhusisha matukio ya namna hiyo na imani za kishirikina.

Huku akiwataka wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa kufuata maelekezo ya Wataalamu juu ya kuto kula nyama ya ng’ombe,iliopigwa na radi ikiwa ni pamoja na kutojaribu kufukua mizoga yale kwa njia za kificho kwa lengo la kujipatia kitoweo kwani watakua wanahatarisha afya zao.