January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rukwa waanzisha utalii wa nyuki

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa,imeanzisha utalii wa nyuki,ambao utamp fursa mtalii kujionea shughuli za ufugaji nyuki katika hifadhi ya mazingira asilia Kalambo.

Pia atapata fursa ya kudungishwa nyuki mwilini ili kuchochea na kuimarisha kinga za mwili kwa watalii ambao watakuwa wakitembelea hifadhi hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utalii huo Askari wa uhifadhi wa TFS Kalambo, Daniel Dotto,amesema katika kufanisha hilo Serikali imeanzisha shamba maalum kwa ajili ya ufugaji nyuki na kutoa mizinga 500 yenye thamani ya millioni 150 ambayo itawezesha watalii kujifunza namna bora ya ufugaji wa nyuki kisasa.

Amesema pia mtalii ataweza kujionea mazingira halisi ya ufugaji nyuki na mazingira ya ikolojia ya msitu huo ikiwa ni pamoja na kutembelea maanguko ya maji ya mto Kalambo ambayo ni ya pili Afrika kwa urefu wa mita 235 kutoka maji yanapoanzia.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa TFS Ibrahim Mkiwa,amesema uwepo wa utalii huo utawezesha kuongezeka kwa mapato ya Serikali pamoja na watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, ambao kwa sasa wamefikia 1000 kwa mwaka,huku akiwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili kujionea na kujifunza namna bora ya utengenezaji wa mizinga na ufugaji nyuki kisasa.

Hata hivyo uanzishwaji wa utalii huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha wawekezaji na watalii kutembelea vivutio vya ndani.