Fresha Kinasa, TimesMajiraOnline,Mara.
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kupambana na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia Mkoani Mara limewaaga na kuanza kuwarudisha katika familia zao Mkoani humo Wasichana 88 kati ya 271, waliokuwa wakipatiwa hifadhi na vituo vinavyomilikiwa na Shirika hilo baada ya kukimbia kufanyiwa ukeketaji mwezi Desemba 2024. Huku 183, wakisalia vituoni kutokana na Wazazi wao kutokuwa tayari kuwapokea.
Hafla ya kufunga kambi na kuwaaga Wasichana hao imefanyika Januari 11, 2025 Kiabakari Wilaya ya Butiama ambapo waliokuwa wakipatiwa hifadhi katika kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama ni wasichana 156, na wanaorudishwa nyumbani ni 50 na Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kilichopo Wilayani Serengeti kilikuwa na Wasichana 115, wanaorudishwa ni 38.
Wakiwa katika vituo hivyo,wameweza kupata hifadhi kwa kipindi cha mwezi mmoja, kupewa mahitaji muhimu, pia kufundishwa mambo mbalimbali ikiwemo madhara ya ukatili, kupewa msaada wa Kisaikolojia, afya ya uzazi, kujitambua, masomo ya ziada (Tuition) na haki zao.
Uamzi wa kuwarejesha makwao Wasichana hao 88,unakuja kufuatia mazungumzo ya pamoja baina ya Viongozi wa Shirika hilo kupitia Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly, Viongozi wa serikali na Wazazi wa mabinti hao ambao wamekubali kuwapokea na kukiri kutowafanyia kitendo hicho badala yake watawasimamia waendelee na masomo yao kwa faida yao na Taifa kwa siku za usoni.
Wasichana 183, wanaosalia katika vituo hivyo Wazazi wao bado hawajawa tayari kuwapokea na mazungumzo ya pamoja bado yanaendelea kufanywa na kwamba, wataendelea kusalia katika vituo hivyo huku wakiendelea na masomo yao ya elimu na ufundi kwa wale ambao hawako katika mfumo rasmi wa elimu kusudi wapate ujuzi utakaowaingizia vipato katika maisha yao.
Aminani Mfinanga ni Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Butiama akizungumza wakati wa kuwaaga Wasichana hao, amemshukuru Mkurugenzi wa Shirika hilo Rhobi Samwelly kwa kuwapa hifadhi Wasichana hao, mahitaji yao pamoja na elimu ambayo itakuwa msingi thabiti katika kuwafanya wajiamini. Huku akitoa wito kwa Wazazi na walezi kutowakeketa Wasichana pia kuachana na mila na desturi zenye madhara.
Pia, amewataka Wasichana hao wawapo katika familia zao, wawe makini kubaini njia na viashiria ambavyo Wazazi na walezi wao watavionesha na kama vitalenga kuwakeketa watoe taarifa haraka katika Ofisi za Serikali za Vijiji, Polisi, Ofisi za Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya hatua za kisheria kudhibiti kufanyiwa ukatili.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly amesema iwapo baadhi ya Wazazi na walezi watashindwa kutekeleza wajibu wao wa kuwalinda Watoto hao na kutaka kuwakeketa watawapokea kwa upya wasichana hao lengo ni kutaka waishi salama na wasome kikamilifu kusudi watimize ndoto zao.
“Katumieni vyema fursa ya kusoma kusudi mtimize ndoto zenu, Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua vyema chini ya Rais makini na mahiri Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye dhamira yake ni kuona kila mtoto Mtanzania anasoma. Iwapo baadhi ya Wazazi watakaidi na kutaka kuwakeketa kwa siri mkija vituoni tutawapokea tunataka msifanyiwe ukatili bali msome kwa ufanisi.” amesema Rhobi.
Wasichana hao kwa nyakati tofauti wametoa shukrani zao za dhati kwa Mkurugenzi huyo Rhobi Samwelly kwa kujitolea kwake na kusimama pamoja nao kuwapa hifadhi na huduma zote muhimu kwa kipindi chote ambacho wamekuwa katika vituo hivyo. Pia wakaahidi kuwa sehemu ya kuunga mkono mapambano ya ukatili katika Jamii.
More Stories
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
Sherehe Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar zafana
Simbachawene:Waombaji wa ajira jiungeni na Mfumo wa Ajira Portal