January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simbachawene:Waombaji wa ajira jiungeni na Mfumo wa Ajira Portal

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imewataka waombaji wa ajira Serikalini kujiunga na Mfumo wa Serikali wa Ajira Portal utakaowawezesha kuoata taarifa ya nafasi za kila kila zinapotangazwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna waombaji wa ajira wanavyoweza kupata taarifa ya nafasi za kazi mara tu baada ya kutangazwa na Serikali .

Amesema, kujiunga na mifumo hiyo kutawasaidia waombaji kujisajili na kufuatilia maendeleo ya maombi yao kwa urahisi .

Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa uwazi na ufanisi katika mchakato wa ajira, akisema ni lazima waombaji wafuate miongozo na kutumia teknolojia ili kuongeza nafasi zao za kupata kazi.

Aidha amesema ,Serikali inafanya juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza nafasi za ajira.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka vijana kujiandaa vizuri kwa ajili ya soko la ajira kupitia mafunzo na ujuzi wa kisasa, huku akiwashauri waombaji kuwa na subira katika kutafuta ajira, kwani serikali ina nia ya kutoa fursa zaidi kwa wananchi.

Waziri Simbachawene amefafanua kuwa Sekretarieti ya Ajira inatekeleza mchakato wa kuajiriwa kwa njia ya kidigitali kupitia “Ajira Portal”, ambapo waombaji wanatuma maombi yao mtandaoni na kupata mrejesho wa papo hapo na Mchakato huu unajumuisha hatua tatu ambazo ni usaili wa kuandika, usaili wa vitendo, na usaili wa mahojiano.

Aidha, ametangaza kuwa kuanzia Januari 14 hadi Februari 24, 2025, usaili wa kada za Ualimu utafanyika nchini, ukilenga kujaza nafasi 14,648 ambapo Usaili huo utahusisha waombaji kufanya mtihani katika mikoa yao, hivyo kupunguza gharama za usafiri.

” Waombaji wanatakiwa kuhuisha taarifa zao katika Ajira Portal na kubeba vyeti vyao halisi siku ya usaili” Amesema