Na Penina Malundo,Timesmajira
Asasi za kiraia (AZAKI) zimependekeza kwa serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050,kuhakikisha sekta ya elimu nchini inakuwa ni moja ya sekta za kimapinduzi ili kusaidia utekelezaji wa Dira uendane na wakati.
Akizungumza katika Mkutano wa Asasi za Kiraia (Azaki) kuhakiki rasimu ya dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mjumbe wa Kikosi kazi cha Mapitio ya Dira hiyo ,Nuru Marwa amesema kupitia dira hiyo,sekta ya Elimu haijawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi wakati dira hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda.
Amesema kutokana na teknolojia inakua kwa kasi na ndiyo nyenzo kuu ya uzalishaji na tija katika nchi ambayo idadi kubwa ya watu wako chini ya umri wa miaka 15, matumizi na uzalishaji wao wa kidijitali vinapaswa kuzingatiwa kupita makuzi yao ya kielimu.
Amesema wanaipongeza serikali kwa utoaji wa Dira kwani imetoa mpango wa utekelezaji ambapo ikifika wakati wa tathmini ya utekelezaji wa Dira ya maendeleo utolewe kupitia data.
“Dira hii ni nyenzo muhimu kwa upangaji wa pamoja wa ndoto za Watanzania kama Taifa ambapo kupitia Dira, Watanzania wanaweka bayana matarajio na mipango yao juu ya Tanzania waitakayo katika miaka 25 ijayo.
“Tumekaa kama Azaki na kutoa miongoni mwa mapendekezo ambayo tuneyachambua na kuona leo tuyalete katika kamati hii ni pamoja na kutoshahibiana kwa maudhui pamoja na data kwenye chapisho la Kiswahili na Kingereza katika Dira hii,”amesema.
Ametolea mfano katika ukurasa 2.1 unaoeleza Uchumi Imara, Jumuishi na shindani, aya ya kwanza kwenye utangulizi upo tofauti na chapisho la Kingereza ambapo kasi ya kukua kwa uchumi ni asilimia 6.4 wakati ya kiingereza ni asilimia 5-6.7.
Amesema katika hilo Azaki imependekeza kwamba kamati itumie taarifa na takwimu sahihi na za aina moja kwenye nyaraka zote mbili.
“Katika suala la Utawala na Uongozi bora haujawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi hivyo tunapendekeza, Utawala na Uongozi bora kama moja ya sekta za kimkakati, kwani ukitaka maendeleo unahitaji watu, ardhi, uongozi bora na siasa safi ili kufikia maendeleo tunayotarajia.
Kwa upande wake mjumbe wa Kikosi kazi hicho,Deus Kibamba amesema wamependekeza kuingiza mpango wa bima ya afya kwa wote kuwa sehemu ya matarajio katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Amesema Dira inatakiwa kuweka wazi kuwa, bima ya afya kwa wote itakuwa nafuu, yenye tija na ufanisi kwa makundi ya watoto,wazee, wanawake, wanaume pamoja na watu wenye ulemavu.
Kibamba amesema utekelezaji wa hilo utaiweka nchi katika orodha ya nchi zilizofanikiwa katika utoaji wa huduma hiyo ulimwenguni.
“Serikali ipo katika mkakati wa kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote kwa ufanisi zaidi hivyo suala hili halitakiwi kusahaulika katika dira ya maendeleo 2025”amesema.
More Stories
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia