January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajawazito 140, wapatiwa vifaa vya kujifungulia

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Chato

Wajawazito zaidi ya 140, wilayani Chato, mkoani Geita,wamenufaika na vifaa vya uzazi vyenye thamani ya milioni 7, vilivyotolewa na na taasisi ya The Desk & Chair kwa ufadhili wa kikundi cha NUDBA cha Toronto,nchini Canada.Ambapo kikundi hicho kikiadhimisha miaka 20, tangu kuanzishwa.

Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation,Alhaji Dkt.Sibtain Meghjee,amesema kuwa, msaada huo utawapunguzia changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujifungulia wajawazito wenye hali duni kimaisha na wasio na uwezo kiuchumi.


“Kutokana na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujifungulia wajawazito katika vituo vya kutolea huduma za afya, Wilaya iliomba vifaa hivyo katika taasisi yetu,hivyo tumewakabidhi viwasaidie,”amesema .

kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato (DAS),Thomas Dime,amesema msaada huo wa vifaa vya uzazi,vitawasaidia wajawazito zaidi ya 140 wanaotarajia kujifungua.


“The Desk & Chair Foundation,ni marafiki wa kweli,wamekuwa wakituletea msaada wa viti mwendo.Kwa niaba ya uongozi wa Wilaya ya Chato,niwapongeze na kuwashukuru, mkumbe Chato ni eneo lenu la kazi, endeleeni kutuunga mkono,”amesema.

Muuguzi wa Kituo cha Afya Bwanga,Enice Mwavika, amesema kituo hicho kwa mwezi kinahudumia wajawazito 550 hadi 600,lakini wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za kufanya maandalizi kabla ya kujifungua,sababu wanatoka familia duni kimaisha.

Mwavika amesema, kwa sababu hiyo baadhi yao hulazimika kutumia vifaa duni visivyo salama, ambavyo vinahatarisha afya na usalama wao.


Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto Wilaya ya Chato,Hezron Yuda,kwa mwezi wanahudumia wajawazito kati ya 1800 hadi 2000, katika vituo 41 vya kutolea huduma.

“Tunashukuru msaada huu wa “delivery park” (vifaa vya kujifungulia), vitawasaidia wajawazito wanapokwenda kujifungua,hii inashiria kuwa mama wa uchumi wa chini wasio na uwezo wa kupata vifaa hivyo, wamepata neema,”amesema.

Yuda amesema vifaa hivyo vitaongeza chachu kwa wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea tiba,huduma bora za afya ya uzazi na kuomba wadau kuendelea kusaidia ili kukidhi mahitaji ya vituo 41 mbali na vinne vilivyonufaika.

“Vituo vilivyonufaika kwa msaada huo ni vya Bwanga 60, Mapinduzi 20,Buseresere 50 na Hospitali ya Wilaya 10.Tukipata msaada zaidi tutaongeza chachu,endeleeni kutusaidia ili kuwafikia wanawake wengi.Tumefarijika kwa kugusa huduma ya afya ya mama na mtoto,”amesema.


Baadhi ya wajawazito wameomba juhudi zaidi zifanyike kwa wadau mbalimbali kusaidia vifaa hivyo kuepuka kutumia vifaa duni visivyo salama wakati wa kujifungua.