January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CP.Wakulyamba ashuka Katavi na Nguzo nne za Uongozi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendeleza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la maboresho ya Jeshi la Uhifadhi kwa kuzingatia maoni ya Kamati ya Haki Jinai kwa kulijengea uwezo Jeshi hilo Kanda ya Magharibi kupitia mafunzo maalum yanayoshirikisha wakufunzi wabobezi kutoka Jeshi la Polisi.

Akizungumza na Maafisa na askari wa Jeshi hilo waliopo chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mkoa wa Katavi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amesisitiza weledi katika kutekeleza majukumu yao.

Awali akiongea na Maafisa wa Jeshi hilo Kanda ya Magharibi, CP. Wakulyamba amewasisitizia kufanya kazi kwa kuzingatia mambo manne ya msingi katika uongozi ili waweze kusimamia vyema majukumu ya ulinzi wa Maliasili katika maeneo yao.

Aidha CP. Wakulyamba ameyataja mambo hayo kuwa ni Kujiamini kwa kuwa Serikali imewaamini na kuwapa dhamana ya kusimamia maliasili, jambo la pili ni uadilifu utakaowapa nguvu ya kusimamia maadili kwa askari wanaowaongoza.

Jambo la tatu ni kusimamia misingi ya kazi kwa haki na siyo kumwonea mtumishi na la nne ni Utawala wa Himaya ambapo amesema kila mtu kama kiongozi ana wajibu wa kuyafahamu vyema maeneo yake ya kazi na kuyasimamia ipasavyo jambo litakalopelekea ufanisi katika usalama wa Maliasili katika Mkoa huo.

Akiongea na askari wa Uhifadhi Mkoa wa Katavi, CP. Wakulyamba amesema, Kanda ya Magharibi imebarikiwa kuwa na maeneo muhimu yaliyohifadhiwa kisheria hivyo ni lazima wayalinde maeneo hayo kwa taratibu zilizopo na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria, kwa maslai mapana ya Taifa.Kwa mujibu wa Kamanda wa Kanda ya Magharibi TFS, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Uhifadhi, Ebrantino Mgiye amesema kuwa rasilimali za Misitu zinazosimamiwa na TFS Kanda ya Magharibi ni pamoja na Hifadhi za Misitu 33 zenye uoto tofauti tofauti katika jumla ya eneo la takribani Kilomita za laki 2.3 sawa Hekta za mraba 4.9 au Ekari 12.3 ikijumuisha Hifadhi ya Mazingira Asilia Itulu Hills yenye eneo la Hekta 388,512.4 (sawa na Ekari 960,035.05).