Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.
MKUU wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko,amesema kitendo cha wakulima wa wilaya ya Tanganyika kufyekewa mahindi kwenye msimu huu wa kilimo sio maelekezo ya serikali na si haki kufanya hivyo.
Mwishoni mwa mwezi Disemba,2024 baadhi ya wakulima wa kijiji cha Kagunga kata ya Kasekese wilayani humo walifyekewa mahindi yao zaidi ya hekari 60 na kutafsiriwa kuwa ni udhoroteshaji wa makusudi wa jitihada za serikali za kuifanya nchi kuwa ghala la chakula Afrika na kutokomeza janga la njaa.
Kiongozi huyo wa juu wa serikali ya mkoa, akizungumza hivi karibuni amebainisha pamoja na nia nzuri iliyopo ya kufanya doria katika misitu, maeneo tengefu na maeneo yaliyo hifadhiwa lakini ufyekaji wa mazao haukubaliki.
Akiwa katika manispaa ya Mpanda akikagua miradi ya maendeleo, Mrindoko ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kuchukua hatua za haraka kulipa fidia ya mbegu kama sehemu ya uharibifu uliojitokeza.
“Ufyekaji wa mazao ni hapana na tulilizungumzia hili wakati uliopita mwaka jana na sasa narudia tena ni marufuku kufyeka mazao ambayo yameshakuwa makubwa na kwa ujumla wake wala si jambo zuri na wala halipendezi,”amesema.
Katika kuhakikisha kitendo cha ufyekaji mahindi haukijitokezi katika maeneo yoyote ya mkoa huo, ametoa wito kwa wakuu wa wilaya ya Tanaganyika, Mlele na Mpanda kuhakikisha doria zinazofanyika katika misitu na mapori tengefu zisihusishe ufyekaji wa mazao ya wananchi.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa imepokelewa kwa shangwe na wakulima wa wilaya ya Tanganyika wakisema imeamsha morali ya wakulima iliyokuwa imefifishwa kwa ufyekaji mahidi huku wakisema ni wakati mwafaka wa viongozi kuongozwa na hekima kwenye kufanya maamuzi yao.
Aisha Hassan, Mkazi wa wilaya ya Tanganyika amesema ufyekaji wa mahindi ulikuwa kinyume na makubaliano kati ya wananchi na serikali ya kijiji huku akiomba agizo la mkuu wa mkoa la kupatiwa mbegu lifanyike kwa wakati mwafaka.
“Tegemeo letu ni kilimo ambacho ni msaada mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wetu na ndio maana serikali inatambua umuhimu huo na inafanya kazi kubwa ya kuweka mazingira wezeshe ya kutukomboa kwenye umasikini kupitia kilimo kama mnavyofahamu serikali inatoa hadi mbolea ya ruzuku” Amesema.
Tungu Shigela amefafanua kuwa wamejipanga kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya chakula unaongezeka zaidi kwani kupitia watalaamu wa kilimo wanapata elimu bora ambayo niwezeshi katika matumizi ya mbolea na mbegu.
Hata hivyo baada ya tukio la ufyekaji wa mahindi, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi Onesmo Buswelu alisema mahindi yaliyofyekwa katika doria hizo ni mahindi na bangi ambazo zililimwa na wavamizi wa misitu ambapo ulizua maswali mengi kwa wananchi wakihoji kama ni bangi ni watuhumiwa wangapi wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kosa la kilimo cha bangi katika eneo hilo.
More Stories
Wananchi Kisondela washukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima