January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Tanga.

MADEREVA bodaboda na bajaji wa Tanga Mjini, kupitia Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Tanga Mjini (UWAPIBATA), wameamua kumchangia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiasi cha shilingi Milioni Moja kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Tukio hili lililoshuhudiwa leo, Januari 4, 2025, lilifanyika katika viwanja vya Lamore jijini Tanga, ambapo Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, alikutana na waendesha pikipiki na bajaji katika jitihada zake za kusikiliza changamoto zao na kujadiliana nao kuhusu maendeleo ya sekta hiyo.

Waendesha bodaboda na bajaji hao walielezea kuridhika kwao na juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge Ummy Mwalimu katika kuboresha mazingira ya kazi zao, akielezea jinsi hatua za kiongozi huyo zilivyogusa maisha yao na kuhamasisha maendeleo katika jimbo la Tanga Mjini.

Katika hatua nyingine, Ummy Mwalimu alichangia shilingi Milioni Kumi katika mfuko wa UWAPIBATA ili kusaidia utekelezaji wa mipango ya umoja huo. Akizungumza baada ya tukio, Ummy alisema, “Bodaboda ni kazi kama kazi nyingine. Mimi kama Mbunge wa Tanga Mjini, nitaendelea kuwathamini na kushirikiana nao ili kuboresha mazingira ya kazi zao. Kipekee, nimevutiwa sana na kitendo cha madereva bodaboda na bajaji kumchangia Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kuchukua fomu ya Urais. Rais Samia amefanya kazi kubwa sana Tanga Mjini, hasa katika maboresho ya Bandari ya Tanga, ambayo yameongeza fursa za biashara kwa madereva bodaboda na bajaji.” Kitendo hicho cha kuonyesha upendo na msaada kwa Rais Samia, kimeonekana kama ishara ya kutambua juhudi za serikali na kuonyesha imani kwa uongozi wake.