Na Mwandishi Wetu, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amesitisha mkutano wa Kanisa la Efatha uliokuwa ufanyike kuanzia jana hadi Aprili mwaka huu, Bungu wilayani Kibaha ikiwa ni tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Corona mkoani hapa.
Akitembelea eneo la mkutano huo akiwa na Kamati ya Usalama Mkoa, alipokea taarifa ya maandalizi ya mkutano huo ikiwa na namna walivyojipanga kuchukua tahadhari ya maambukizi ya Corona.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Vivian Mmari alisema mkutano huo ni wa siku tano na utajumuisha washiriki 3,000 ambao ni viongozi wa mikoa wa kanisa hilo kutoka nchini kote na wamejipanga kujikinga na maambukizi ya Corona ikiwa ni pamoja na kufanya vipimo vya awali na kuwa na vitakasa mikono kila eneo.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Ndikilo alisema; “Mazingira tuliyoyakuta wingi wa watu, mazingira ya kulala, mwingiliano wa watu kutoka mikoa mbalimbali, idadi ya siku za mikutano, kamati ya usalama inatilia shaka kukiukwa kwa maelekezo ya serikali yaliyotolewa ya kuchukua tahadhari na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa na lazima,” alisema.
Aliongeza kuwa lengo si kuzuia ibada ni kuchukua tahadhari madhubuti ya kujikinga na ugonjwa wa Corona, unaoenea kwa kasi.
Licha ya hayo, Mhandisi Ndikilo alisisitiza waumini wa madhehebu yote Mkoa wa Pwani waendelee na ibada kwa siku zao za ibada huku wakichukua tahadhari.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti