Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe.
WADAU wa uchaguzi Mkoa wa Songwe kupitia majukwaa yao ya kisiasa,kijamii,kitamaduni na kiimani, wametakiwa kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi,kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura kama msingi wa uchaguzi bora wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Rai hiyo imetolewa Desemba 31, 2024 na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Uchaguzi, Grayson Orcado, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi Mkoa wa Songwe uliofanyika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ikiwa ni maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mzunguko wa tisa.
Amesema kufanikiwa kwa zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura kwa Mkoa wa Songwe, kutategemea ushiriki wa wadau hao wa uchaguzi katika kutoa elimu na kuhamasisha wanannchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au kuhamisha au kuboresha taarifa zao.
“Matarajio ya Tume,mtakuwa mabalozi wa kusambaza taarifa na kuhamasisha wananchi ili zoezi hili lifanyike kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa,” amesema Orcado.
Pia ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wadau na wananchi kwamba kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha sheria ya uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024.
Amesema mtu yeyote atakayeombwa kujiandikisha zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atakumbana na adhabu ya faini isiyopungua kiasi cha 100,000 na kisichozidi shilingi 300,000 au kifungo kisichopungua miezi sita.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa, Saida Mohammed, akitoa mada katika mkutano huo, amesema wapiga kura wapya 5,586,433 wanatarajia kuandikishwa ,sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura ,29,754 699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka wa 2019/2020.
Amesema wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao huku wapiga kura 594,494 wataondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye daftari, ambapo baada ya uboreshaji, inatarajiwa kuwa daftari la wapiga kura litakuwa na jumla ya wapiga kura, 34.746,638.
Saida ameongeza kuwa, zoezi hilo kwa Mkoa wa Songwe linatarajia kuanza January 12 Hadi 18 mwaka 2025 na kwamba jumla ya wapiga kura wapya 110,803 wataandikishwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya wapiga kura 619,703 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga.
More Stories
Ulega kuwapima Mameneja TANROADS kwa kutatua changamoto
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV