January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasanii wazidi kumiminika JKCI ofa ya Rais Dkt. Samia

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

WASANII wameendelea kuchangamkia fursa ya kupima moyo bure katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa uchunguzi wa moyo kwa wasanii hao jana, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Peter Kisenge, alisema amefurahi kuona wasanii wanachangamkia fursa hiyo na kuwataka wengine kuendelea kujitokeza.

“Nimemwona Zuchu, Mboso, D Voice wamekuja naomba nitumie fursa hii kuwashauri wasanii wengine waige mfano huu wa kuja kupima vipimo vya moyo bure,” alisema

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa fursa hii ya kuwapima wasaniii bure hii ni kuhamasisha wananchi wote wawe na tabia ya kupima afya zao ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanachangia vifo vingi sana,” alisema

Naye Mbwana Yusufu kutoka (WCB), maarufu kama Mboso alisema yeye ana shida ya moyo na amekuwa akifanya vipimo mara kwa mara kujua maendeleo ya afya yake ya moyo.

“Binafsi najifahamu nina matatizo ya moyo na ninaendelea na matibabu madogo madogo, nimefanya vipimo na nimeonekana bado ninashida nitafanyiwa vipimo zaidi na wameahidi kutatua changamoto yangu,” alisema

“Namshukuru sana Rais Samia kwa kutupa fursa hii nawaomba wasanii waje kujua kama wanachangamoto ya moyo wasiogope kwasababu hapa ni vipimo na ukigundulika unashida unapatiwa matibabu,” alisema

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini (BASATA), Dk. Kedmon Mapana aliwashukuru wasanii kwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa na Rais Samia na alimshukuru pia Dkt. Kisenge kwa kufanikisha upimaji huo.

“Tunamshukuru na kumpongeza sana Dk Kisenge kwa kuratibu zoezi hili maana wasanii wamekuwa wakija hapa JKCI na nimeona Diamond akihamasisha wasanii wengi waje na leo ameleta pia kundi la wasanii wa lebo yake,” alisema