December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

VIONGOZI na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),mkoani Tabora wametembelea familia ya mjane wa kada wa chama hicho Jastin Magembe,aliyedaiwa kujiua kwa sumu, baada ya mgombea wao kushindwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Novemba 27,2024.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Kata hiyo,Gabriel Maige, amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 28 mwaka huu siku moja,baada ya kumalizika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo mgombea wao alishindwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora,Komredi Wilson Nkambaku na Wajumbe wa Sekretarieti ya chama Mkoa,wamefika nyumbani kwa marehemu Kitongoji cha Ikomwa Mlimani, Kata ya Ikomwa, Manispaa ya Tabora ili kumfariji mjane huyo na familia ya marehemu,ambaye alikuwa Kampeni Meneja wa mgombea na Mjumbe wa Baraza la UVCCM katani hapo.

Akitoa salamu za pole kwa wafiwa na wanaCCM wote katika Kata hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi, Komredi Nkambaku ameeleza kuwa chama kimepokea kwa masikitiko tukio hilo la kujiua kada wao.

Amebainisha kuwa marehemu alikuwa mwanachama mahiri aliyesimamia vema shughuli za chama,na alitoa mchango kwenye kampeni za uchaguzi huo uliomalizika hivi karibuni ambapo mgombea wa CCM alishindwa.

Amewahikikishia wanafamilia kuwa CCM itaendelea kumuenzi kada wake aliyetangulia mbele za haki,kutokana na mchango aliotoa katika kupigania maslahi ya chama chake na wataendelea kuwa karibu na familia hiyo.

Nkambaku amewasihi wanaCCM na jamii kwa ujumla kuendelea kukiamini chama hicho na kubainisha kuwa hata kama wamepoteza kiti hicho Serikali haitaacha kuwaletea maendeleo.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa huo, Komredi Iddi Moshi Mambo, ameeleza kuwa marehemu Jastin Magembe ni askari mtiifu wa chama aliyefia vitani hivyo CCM,itaendelea kumkumbuka kama shujaa wake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikomwa kwa awamu 2 mfululizo, Magembe John Spemba,ambaye ni baba mzazi wa marehemu amewashukuru sana Viongozi hao kwa kwenda kuwafariji na kuahidi kuwa wataendelea kukitumikia chama chao.