
Na Moses Ng’wat, Tunduma.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Aboubakar Kunenge, leo Novemba 3, 2026, amefungua rasmi matumizi ya njia mbili za barabara ya njia nne katika eneo la Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) Tunduma, hatua inayotarajiwa kupunguza msongamano wa malori na kurahisisha usafirishaji wa mizigo katika mpaka huo.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache,
tangu Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kutoa maelekezo kuhusu kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo, yaliyokwenda sanjari na kutumbuliwa kwa aliyekuwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Frederick Mande
Kunenge amefungua njia hizo baada ya kutembelea eneo la mradi na kukagua maendeleo ya ujenzi, huku akiridhia magari makubwa ya mizigo kuanza kuzitumia baada ya wataalamu kuthibitisha kuwa zege limekomaa na lina uwezo wa kuhimili uzito wa magari hayo.
Akizungumza wakati wa kufungua barabara hiyo, amesema matumizi ya njia hizo yatawezesha magari yanayoingia na kutoka nchini kutumia njia hizo, hivyo kupunguza mwingiliano na msongamano uliokuwa ukikwamisha shughuli za usafirishaji katika mpaka huo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja mpya wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Silvanus Mroka, amesema utekelezaji wa mradi mzima umefikia asilimia 76, huku mkandarasi akiendelea na ujenzi wa kilomita 1.275 zilizobaki kuelekea Mbeya.
Amesema njia mbili zilizobaki zinatarajiwa kufunguliwa Novemba 17, mwaka huu, hatua itakayokamilisha matumizi ya njia zote nne na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kupitia mpaka huo.

Ameongeza kuwa, Sehemu iliyofunguliwa ina urefu wa mita 400 na upana wa mita 14, kuanzia eneo la geti la Nakonde upande wa Zambia hadi mzunguko wa magari (Roundabout) upande wa Tunduma.
Baadhi ya madereva wanaotumia mpaka huo wameipongeza Serikali kwa kufungua njia hizo, wakieleza kuwa zitapunguza muda wa kusubiri, foleni, mizunguko mirefu ya magari na matumizi ya mafuta yaliyokuwa yakiongezeka kutokana na msongamano.
Kunenge amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na kuweka mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji, huku akisisitiza wananchi kutumia fursa hiyo kuifanya Tunduma kuwa kitovu cha biashara na uchumi badala ya kuwa eneo la makazi pekee.


More Stories
Operesheni Star Rating yafungua ukurasa mpya.
Waziri Mkuu wa Rwanda avutiwa na bidhaa za Tanzania
Tanzania yatumia ISA kuvutia Uwekezaji wa Nishati ya Jua