Judith Ferdinand,
Katika siku za karibuni, watoto na vijana wa Kitanzania wamenukuliwa wakiungana na wenzano katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa, kukosoa kile wanachokiita ‘kutengwa’ katika vita ya athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, alhali wao wakiwa ndiyo waathirika wakubwa wa matukio hayo.
Kati ya Septemba na Oktoba 2024 wakiwa sehemu ya mamia ya watoto na vijana kutoka mataifa 20, walioshiriki mikutano ya utangulizi kabla ya kusanyiko la kimataifa la Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) uliofanyika Baku, Azerbaijan, watoto wa Tanzania walitoa mapendekezo kadhaa yanayotuma ujumbe juu ya kutofurahishwa kwao na ushirikishwaji hafifu katika masuala ya tabia nchi.
Mapendekezo ya watoto na vijana wa Tanzania yamejumuishwa na mengine yaliyotolewa makundi ya nchi nyingine 19, katika ripoti ya Shirika la Save the Children iliyopewa jina la “Children’s Climate Demands for COP29,” kwa tafsiri isiyo rasmi ikimaanisha ‘Madai ya watoto kuhusu mabadiliko ya tabianchi kwenye mkutano wa COP29’.
“Lazima kuwe na ushirikishwaji wa maana wa watoto katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutuhusisha katika maandalizi ya mipango, sera, na uwakilishi kwenye kamati zinazoshughulikia mabadiliko ya tabianchi,” insomeka sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza:
“Hii itahakikisha kuwa masuala na sauti za watoto zinasikika na kupewa kipaumbele katika hatua za hali ya hewa.”
Harakati za watoto na vijana hawa zilianza kuingia kwenye kumbukumbu rasmi mwaka 2023 kwenye uzinduzi wa Ripoti ya “Watoto kwa Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi: Sauti kutoka Tanzania” ambayo ilisisitiza umuhimu wa kuingiza mtazamo wa watoto katika suluhisho za mabadiliko ya tabianchi, ikionyesha kwa upande mmoja udhaifu na uwezo wao kwa upande mwingine katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Sauti zao ni kama zimeanza kusikika masikioni mwa watungaji na watekelezaji wa sera kwani ziko hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kulishirikisha kundi hili muhimu la kijamii katika vita hii ambayo imeshika kasi katika maeneo mbalimbali duniani ikilenga kuokoa dunia dhidi ya majanga yanayotokana na uharibifu wa mazingira.
Sauti zinasikika?
Mkoani Mwanza katika shule ya msingi Magaka, iliopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wanawashirikisha wanafunzi wa shule hiyo kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza na Timesmajira Online walisema wanaamini ushirikishwaji huo utawasaidia kufanya vyema kwenye masomo, kwani watapata kivuli, hewa safi, mbao, dawa za asili na kupunguza upepo mkali ambao unaweza kuezua mabati katika madarasa na kusababisha kushindwa kuendelea na masomo.
Angel Chacha ambaye ni Katibu Msaidizi wa Klabu ya Mzaingira ya shule hiyo anasema wanashirikishwa katika upandaji wa miti na kuitunza, kufanya usafi wa mazingira na kufukia baadhi ya maeneo ya shule ambayo udongo wake umemomonyoka kutokana na mvua kubwa.
Kwa upande wake Katibu wa Klabu ya Mazingira wa shule ya msingi Magaka, Fides Samweli anasema kushirikishwa kwako kupanda miti na kutunza mazingira shuleni hapo, ni hatua ya kutengeneza kizazi chenye uelewa wa kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabaianchi.
Kinachofanyika katika shule ya msingi Magaka, kinashabihiana na kile kinachofanywa na shule za msingi za Kawe katika Manispaa ya Kinondoni na Kibondemaji katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambako wanafunzi wanashirikishwa katika shughuli za kuyakabili mabadiliko ya tabia nchi.
Kupitia mradi wa ‘PAMOJA TUNABORESHA ELIMU’ unaofadhiliwa na Shiriki la We World, shule hizo zinawashirikisha wanafunzi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kupitia klabu za mazingira zinazowashirikisha wanafunzi wa marika tofauti.
Katika ripoti “Watoto kwa Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi: Sauti kutoka Tanzania” iliyojumuisha mawazo ya watoto zaidi ya 12,000 katika mikoa ya Mbeya, Kigoma na Zanzibar, limo pendekezo la kuanzishwa kwa klabu za mazingira katika shule, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha watoto na vijana wanashiriki kikamilifu katika suala hilo.
Matokeo ya ripoti hiyo iliyopewa jina la U-Report yanaonyesha kuwa asilimia 60 ya vijana waliyohojiwa waliona kuwa shule zao hazishughulikii ipasavyo mzozo wa tabianchi, huku asilimia 80 wakisema elimu kama hiyo ni muhimu kwa mustakabali endelevu.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Magaka, Mshongo Mmbaga, anasema
wanawafundisha na kuwashirikisha wanafunzi katika suala zima la upandaji miti shuleni na nyumbani, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa sasa ni janga la dunia.
Shule hiyo iilyoianzishwa mwaka 2023 ina wanafunzi 772 kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba, kati yao wasichana ni 373 na wavulana 399.
“Wanafunzi ni wadau wazuri katika upandaji wa miti, na hapa shuleni walikuja wadau kutupatia miti, tuliwakabidhi kila mtoto mti wake ambao aliupanda na kuitunza,na kwa sasa shuleni hapa ipo zaidi ya miti 100 ya matunda na kivuli.”
“Watoto ni watekelezaji wa zuri wa mambo, tuwape kazi watoto ya kupanda miti hata miwili au mitatu ndani ya familia pamoja na kuwafundisha namna ya kuitunza, itasaidia kuondokana na changamoto hiyo,” anasema Mwalimu Mmbaga na kuongeza:
“Kwa jiografia ya Mwanza maeneo yake kuwa na milima na mawe, ipandwe miti ya asili ambayo inaweza kuota vizuri katika maeneo hayo, mfano hata hapa shuleni kuna eneo lina mawe lakini kuna miti ambayo ukiisha ipanda mizizi yake ikapenya haina shida inakuwa vizuri.”
Mamlaka za kiserikali
Ofisa Mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, David Mgunda, amesema njia kuu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kurejesha uoto wa asili katika uso wa dunia na kuifanya kuwa ya kijani.
Hivyo wanachokifanya kwa sasa ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwashirikisha katika suala zima la upandaji miti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Amesema mwaka 2022/2023, miti 39,700, waliipanda katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, zahanati na hospitali na kwa kiasi kidogo maeneo ya wananchi binafsi.
Huku mwaka 2023/2024, miti takribani 40,727, ilipandwa katika taasisi hizo, asilimia 80 ya miti hiyo ilipandwa kwenye shule.
“Walimu waendelee kusimamia klabu za mazingira shuleni huku wanafunzi waendelea kuitunza na kupanda miti katika maeneo ya shule na nyumbani,huku mazingira liwe somo la kujitegemea na lifundishwe kwa vitendo zaidi.”
Changamoto
Mwalimu Mmbaga amesema licha ya jitihada za kupanda miti, kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na shule hiyo kuingiza mifugo ambayo ina kula majani ya miti na wakati mwingine kuiiba, kwa sababu ya kutokuwa na uzio shuleni hapo.
Hata hivyo amesema hatua walizochukua kukabiliana na changamoto hiyo wameajiri mlinzi ambaye anaimarisha ulinzi shuleni hapo huku wakiiomba Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na wadau mbalimbali kuwasaidia kujenga uzio.
Ofisa Elimu Watu Wazima Divisheni ya awali na msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Magembe Masalu, amesema kuwafanya watoto kuwa sehemu ya mabadiliko ya tabianchi kunaweza kusaidia kufanikisha jambo hilo.
“Kwanza kuwafundisha wakatambua namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo, kwa kujua kitu gani kinatakiwa kifanyike na wao wakashiriki hasa kufanya mambo ya usafi wa mazingira,upandaji wa miti na maua hasa kwenye maeneo ya shule na nyumbani.
“Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, tumeanza mchakato wa uboreshaji na utunzaji wa mazingira kwa kushirikisha wananfunzi/watoto, kupanda miti. Kila mwaka tunajitahidi kupanda miti zaidi ya miche 10,000 kwenye maeneo yetu ya taasisi za elimu msingi na sekondari,” anasema Masalu.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mashelo Makila, anasema wanawasisistiza watoto na vijana kupanda miti kuanzia shuleni na kwenye familia zao na kwama kuna upumuhu wa suala hilo kuwekewa mkazo wa kisera na kisheria.
“Sheria iwepo ambayo ina lazima kila familia inakuwa na miti angalau mitatu ambayo wameipanda ili kuhakikisha mabadiliko ya tabianchi yanaondoka, kwa kufanya hivyo itatoka kwenye sheria na kuwa sehemu ya maisha kama tabia, tamaduni ya watu kujijengea kuwa na miti katika maeneo yao na kuitunza tangu wakiwa wadogo,”anasema.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika