Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib, amesema malezi ya watoto yatima ni jukumu la jamii yote, ili kuwajengea mazingira bora ya maisha.
Mama Zainab ambaye pia ni Mwenyekiti wa ‘Nuru Foundation’ ya Zanzibar, ameyasema hayo leo Disemba 22, 2024, katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya Skuli na madrasa kwa watoto yatima, iliyoandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Kiislamu wa Elimu, Uchumi na Maendeleo (UKUEM), huko katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Saateni, Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.
Mama Zainab amewakumbusha wanawake wanaoishi na watoto yatima na wenye ulemavu, kujikita katika maadili mema, malezi bora na kuepuka kuwatumia watoto hao katika kuomba omba, kwani ni taathira mbaya wanayo wajengea.
“Wapo Wanawake wenzetu wanaotumia sababu ya watoto yatima na wenye ulemavu kupita wakiomba, hakika hili sio jambo jema” amesisitiza Mwenyekiti huyo wa Nuru Foundation.
Aidha ameitaka jamii kujitokeza katika kuchangia gharama za malezi ya watoto yatima, kwa wenye uwezo, ili kuwapunguzia ukali wa maisha.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Amirat Bi. Latifa Abdallah, akitoa ukaribisho kwa wageni na hadhara hiyo, amesema “hafla na mkusanyiko wa namna hii, na hasa ukihudhuriwa na viongozi wetu, inatujengea imani na morali katika kuwasaidia watoto yatima na jamii kwa ujumla”, amesema hayo huku akimshukuru Mama Zainab kwa kuungana nao katika hafla hiyo.
Akiwasilisha ripoti ya Mfuko wa Mayatima ya mwaka 2024, Mwenyekiti wa Mpango wa Udhamini wa mayatima Bi. Arusi Masheko, amesema takriban shilingi Milioni 25,106,100, ambayo ni sawa na asilimia 74 ya makadirio yao, zimekusanywa kupitia vyanzo mbali mbali, na ambazo pia zitakidhi mahitaji ya vifaa vya mayatima 147 kati ya 200 waliokusudiwa.
Miongoni vifaa vilivyotolewa ni; sare za skuli na za madrasa, vifaa vya kuandikia, viatu vya skuli na madrasa, mikoba ya skuli na madrasa pamoja na fedha za matumizi.
Hafla hiyo pia imeshuhudia Nashid, utenzi na harambee kwaajili ya kusaidia watoto yatima, ambapo Mama Zainab amechangia kiasi cha shilingi milioni mbili na laki mbili na sitini elfu ( 2,260,000), kwaajili ya kusaidia ununuzi wa vifaa vya watoto yatima hamsini (50).
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari