Na Agnes Alcardo,Timesmajiraonline.Dar
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) Desemba 18 imeteketeza kilogramu 614.12 za dawa za kulevya katika kiwanda cha saruji cha Twiga, kilichopo Wazo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika tukio hilo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, amesema kuwa, kati ya dawa zilizoteketezwa, kilogramu 601.87 ni methamphetamine na kilogramu 12.25 ni heroin, ambazo zilikuwa zinashikiliwa kama vielelezo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha na Kisutu ambazo ziliamuru uteketezaji wake kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo wakati kesi zikiwa bado zinaendelea.
“Uteketezaji wa dawa hizi unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kanuni zake, sheria hii inaruhusu uteketezaji wa dawa hizi kufanyika kabla, wakati au baada ya shauri kumalizika mahakamani,” ameeleza Kamishna Lyimo.
Pia, Kamishna alifafanua kuwa uteketezaji huo unafanywa kwa njia zinazozingatia usalama wa afya ya watu na utunzaji wa mazingira, huku ukisimamiwa na wadau mbalimbali waliotajwa kisheria.
Aidha, Kamishna Lyimo alibainisha kuwa katika mwezi huu wa Desemba pekee, mamlaka imefanikiwa kuteketeza ekari 12 za mashamba ya bangi katika mkoa wa Tabora, pamoja na kilogramu 398.105 za dawa mbalimbali mkoani Mtwara. Huku pia mamlaka inatarajia kuteketeza kilo 126.21 za mirungi mkoani Arusha katika siku chache zijazo.
Aidha Kamishna Lyimo amewapongeza wadau wote waliofanikisha uteketezaji wa dawa hizo na kuendelea kushirikiana na mamlaka katika juhudi za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya na kuhitimisha kwa kusema kuwa zoezi la uteketezaji litaendelea nchi nzima, kadri mahakama zitakavyoendelea kutoa amri.
“Tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa dawa hizi haramu zinadhibitiwa kwa ustawi wa jamii yetu,” ameongeza.
More Stories
RC Mrindoko:Vyombo vya haki jinai shirikianeni kumaliza kesi kwa wakati
RC Katavi ataka huduma ya maji safi na salama iimarishwe kudhibiti Kipindupindu
Walengwa TASAF Korogwe TC watakiwa kuchangamkia fursa