Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar
MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amewataka wenyeviti wote wa Serikali za mitaa wilayani humo kutochongesha mihuri na kutumika katika kuwahudumia wananchi, mpaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itakapotoa mwongozo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema, halmashauri hiyo ya jiji ndiyo itakayo toa mihuri itakayotumika katika ofisi hizo na kusema kuwa endapo mwenyekiti yoyote wa Mtaa atabainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwani ni kinyume cha sheria.
Mpogolo ameyasema hayo leo Desemba 18, 2024 alipokuwa akifunga semina ya kuwajengea uelewa wenyeviti wapya wa mitaa 159 ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Amesema, mihuri ni nyaraka ya Serikali hivyo Serikali ndiyo yenye mamlaka ya kuiandaa na kuikabidhi kwa watumishi wake kwaajili ya kuwahudumia wananchi.
“Ninawaomba kama kuna waliochinga mihuri wairudishe au waifungie wasiitumie. Tupate mwongozo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , tupate mwongozo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa ambaye ataleta maelekezo,”ameeleza Mpogolo.
Pia amesema mihuri hiyo itaanza kutumiwa na wenyeviti wa serikali za mitaa mpaka pale watakapopewa miongozo na mamlaka husika na siyo vinginevyo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wenyeviti hao kuendelea kuwahudumia wananchi kikamilifu na kuimarisha uhusiano.“Naomba tusichomoke nje ya sheria, tuache matamanio tufuate maelekezo, kama kuna barua unaandika nenda kaiandike halafu mpelekee Afisa Mtendaji agonge muhuri,”alieleza.
Pia,amewakumbusha wenyeviti hao kuwa, barua zote wanazo idhinisha na kugonga mihuri nyingi zina kwenda katika Ofisi za Serikali hivyo wajihadhari na matumizi ya mihuri iliyo kinyume na utaratibu.
“Tuvute subira muda siyo mrefu tutapata maelekezo na tutaishi katika maelekezo, ni wajibu wangu kuwalinda nyie Msitamani kufanya jambo litakalo wapeleka katika kifungo,”ameeleza Mpogolo.
Sambamba na hayo, amewataka wenyeviti hao kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali, miradi inayo tekelezwa katika maeneo yao na kuimarisha uhusiano wao na Serikali.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani,amewataka wenyeviti hao,kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi na kutambua ni wakati gani wanakuwa upande wa wananchi na wakati gani kuwa upande wa Serikali.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mustafa, Kata ya Pugu, Fikiri Rajabu ‘Timbwa’ amesema semina hiyo imewapa mwanga wa uongozi na namna bora ya kuwatumikia wananchi.
“Tumepata semina ya siku tatu, juzi tulikutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa ngazi ya mkoa na jana tulianza semina ngazi ya wilaya na semina zimetupa maelekezo mazuri, tumejijenga kutumikia wananchi, kuwa rafiki na kiungo muhimu baina ya na Serikali na wananchi katika mitaa yetu,”amesema Timbwa.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang