Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
WALIMU Wakuu,Maofisa Elimu Kata, Bodi za shule, Wazazi na Walezi mkoani Tabora,wametakiwa kuwapa kipaumbele watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wanawake wataalamu kwenye sekta mbalimbali.
Wito huo umetolewa leo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt.Huruma Bwageko,wakati akizungumza alipokuwa na waandishi wa habari baada ya kuhitimishwa mafunzo ya siku 1 ya kuhamasisha wasichana kusoma sayansi wilayani Nzega.
Amesema,wana nafasi kubwa ya kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi na sio wa kuwakatisha tamaa.Kwani wasichana walio wengi shuleni hawapendi kusoma masomo hayo kwa hofu kuwa ni magumu, jambo ambalo sio sahihi, .
Dkt. Huruma ambaye ni Mwezeshaji Kiongozi wa mafunzo hayo yanayoratibiwa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) kupitia mradi wa EAGL (Every Adult Girl Learn) amesisitiza kuwa wasichana wanaweza kusoma masomo ya sayansi hivyo wahamasishwe.
‘Watoto wa kike hawajahamasishwa ipasavyo kusoma masomo ya sayansi, tafiti zinaonesha kuwa katika kila watoto 5 wa kike wanaosoma sekondari 1 tu ndiye anasoma masomo hayo, hii sio haki’, ameeleza.
Mratibu wa Shirika hilo wilayani Nzega Flora Shiwa amepongeza UNICEF kwa kushirikiana na Serikali ya Canada na Tanzania kwa kufadhili mafunzo hayo kwa walimu wakuu, maofisa elimu, wenyeviti wa bodi za shule na wazazi zaidi ya 100.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu nzuri zinazoendelea kutolewa na shirika hilo katika Mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe ili kuhamasisha watoto wa kike waliopo katika shule za sekondari kupenda sayansi.
‘Hadi sasa walimu wa sayansi 198 kutoka shule za sekondari 36 wilayani humo wameshapewa mafunzo hayo ambayo pia yanatolewa katika halmashauri zote 8 za Mkoa huo’, amefafanua.
Shiwa ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanahamasisha usomaji na ujifunzaji masomo ya sayansi yaani STUH (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati), kufanikisha hili klabu za masomo ya sayansi zimeanzishwa.
More Stories
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid kuweka kambi Kilosa
NHIF yarejesha Toto Afya Kadi ,yazindua vifurushi vipya
Wanafunzi Tusiime waanza ziara nchini Uturuki