Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
HALMASHAURI ya manispaa Tabora inatarajiwa kunufaika na miradi mitatu ya kimkakati inayotekelezwa na Mfuko wa Benki ya Dunia (WB) kupitia mradi wa TACTIC yote ikiwa na thamani ya zaidi ya sh bil 19.
Miradi hiyo ni ujenzi wa stendi kuu ya kisasa ya mabasi ya kwenda mikoani inayojengwa eneo la Inala Kata ya Ndevelwa Mjini hapa, soko kuu la kisasa linalojengwa katikati ya Mji na barabara za lami zenye urefu wa zaidi ya km 10.
Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Kapela,wakati akizungumza na mwandishi wa wa habari hii ofisini kwake.
Amesema kuwa maandalizi ya utekelezaji miradi ya soko kuu na stendi kuu ya mabasi ya kwenda mikoani tayari yamekamilika, wakandarasi wameshapatikana na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
Mstahiki Meya amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa km 10.7 katika mitaa mbalimbali ya Manispaa hiyo tayari umeanza, mkandarasi anaendelea na utekelezaji.
‘Wafanyabiashara wote waliopo eneo la soko kuu walishirikishwa katika hatua zote kwenye maandalizi ya utekelezwaji mradi huo, walipewa muda wa kutosha kujiandaa kuhama eneo hilo kwa muda kupisha utekelezwaji mradi huo’, ameeleza.
Amesisitiza kuwa wafanyabiashara wote waliopo eneo hilo wanapaswa kuwa wameondoka ifikapo Januari 1, 2025 ili kumpisha mkandarasi kuanza kazi yake, manispaa tayari imeandaa maeneo yatakayotumiwa na wafanyabiashara kwa muda.
‘Kuanza kwa ujenzi wa mradi wa Soko Kuu kunaenda sambamba na ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi, maandalizi ya utekelezaji mradi huu nayo yamekamilika, miradi hii itakapokamilika itaing’arisha halmashauri ya manispaa yetu’, alibainisha.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Manispaa hiyo Shaban Malunda amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Elias Kayandabila na Wataalamu wake kwa kubuni mradi huo na kuwatengea maeneo ili kupisha utekelezwaji wake.
Ameeleza kuwa wako tayari kupisha mkandarasi ili aanze kazi yake na kuahidi kuwa watatoa ushirikiano wa kutosha, aliomba mradi utakapokamilika kila mfanyabiashara apate nafasi ya kufanyia kazi yake pasipo usumbufu wowote.
More Stories
Prof.Muhongo atunukiwa tuzo ya pongezi Musoma Vijijini
PPAA yaokoa bilioni 583
CCM Katavi yakanusha uwepo wa viongozi kuleta wagombea kipindi cha uchaguzi