December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi zaidi ya 350,000 wapata maji safi

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Kaliua

WAKAZI 359,577 wa vitongoji, vijiji na Kata mbalimbali wilayani Kaliua mkoani Tabora wamenufaika na miradi ya maji iliyotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Hayo yamebainishwa na Meneja wa RUWASA wilayani humo,Mhandisi Mapambano Boniface,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama kwa wananchi katika kikao cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo.

Amesema wakazi wanaopata huduma ya maji safi hadi sasa ni zaidi ya asilimia 53 ya wakazi wote wa Wilaya hiyo wapatao 678,447,na maeneo yote ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo ipo miradi inayoendelea kutekelezwa.

Ameeleza kuwa mahitaji ya maji wilayani humo yanakadiriwa kufikia lita za ujazo milioni 14.4 kwa siku, huku hali ya upatikanaji huduma imefikia asilimia 53 ambayo ni sawa na uzalishaji wa lita milioni 7.6 kwa siku.

“Miradi zaidi ya 13 ipo katika hatua za utekelezaji katika maeneo mbalimbali na mingine mipya inayogharimu zaidi ya bilioni 2.6 ,inatarajiwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2024/2025,”.

Mhandisi Boniface amedokeza kuwa miradi hiyo itakapokamilika upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Wilaya hiyo utaongezeka hadi kufikia asilimia 79 ifikapo Juni mwakani.

Katika kukabiliana na changamoto ya maji kwa baadhi ya vitongoji, vijiji na Kata katika Wilaya hiyo,amesema wanatarajia kutekeleza miradi ya uchimbaji visima na mabwawa ya maji ikiwemo kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi.

“Tumepokea kiasi cha milioni 598.9 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la maji katika Kata ya Ichemba ambalo linatarajiwa kufikisha huduma ya maji safi kwa wakazi wa vijiji 28, kupitia mradi huo wakazi zaidi ya 143,000 watanufaika,” ameeleza.

Ametaja baadhi ya miradi iliyopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kuwa ni wa Kijiji cha Usimba, Kombe, Selelii, utafiti wa maji chini ya ardhi sambamba na uchimbaji visima 25 katika vijiji zaidi ya 20 unaogharimu milioni 550.

Mingine ni upanuzi mradi wa maji katika Kijiji cha Kashishi kwenda Kagera, Kijiji cha Kazaroho kwenda Nsimbo, ukarabati visima 70 kwa kubadilisha vipuri, usanifu wa Bwawa la Maji katika Kijiji cha Zugimlole na utafiti na uchimbaji visima 10 katika Majimbo ya Kaliua na Ulyankulu.