December 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askari wanaojihusisha na vitendo vya rushwa wanavyochefua Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAKATI fulani, Rais Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumza Ikulu, jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua alisema;

“Tunataka kuondoa trafiki ili kuondoa rushwa, tuweke kamera.” Kauli hiyo ya Rais Samia inaonesha wazi kwamba anakwerwa na rushwa kwa matrafiki.

Lakini pia tangu aingie madarakani amekuwa akikemea vitendo vya rushwa ndani ya jeshi la Polisi pamoja ameendelea kufanya maboresho mbalimbali.

Jitihada hizo hizo za Rais Samia zimekuwa zikiungwa mkono na Watanzania, wengi ambapo ilikuwa moja na sababu ya kuunda Tume ya Haki Jinai.

Rais Samia, ameweka hadharani jinsi Polisi wamekuwa wakiomba rushwa wananchi, kubambikia wananchi kesi pamoja na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Katika uongozi wake, Rais Samia ameonesha wazi kukemea rushwa ndani ya Polisi kutoka chini ya sakafu ya moyo wake. Huko nyuma amewahi kutoa mfano wa yale yaliyowahi kumkuta ndani ya Jeshi la Polisi.

Lakini pia, Agosti 25, 2021 miezi michache baada ya kuingia madarakani, Rais Samia, alirudia kuliagiza Jeshi la Polisi kukomesha tabia za baadhi ya askari wake hususan wa Usalama Barabarini kupokea rushwa kwenye magari.

Rais Samia alitoa agizo hilo wakati akifungua Kikao Kazi cha Maofisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, huku akisisiza kuwa vitendo vya baadhi ya maofisa wa Jeshi hilo kuomba na kupokea rushwa ni aibu.

Katika hilo, Rais Samia alisema baadhi ya maofisa kujihusisha na vitendo hivyo ni ukosefu wa maadili na kukiuka kiapo cha kazi yao.

Aidha, aliweka wazi kwamba zipo video fupi ‘video clips’ nyingi ambazo zimekuwa zikizunguka ndani na nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii zikionesha baadhi ya maaskari wa Jeshi la Polisi hususan ‘matrafiki’ wakiomba na kupokea rushwa kwenye magari.

Pamoja na kukemea Rushwa, Rais Samia ameendelea kufanya maboresho mbalimbali ndani ya jeshi hilo. Hata hivyo, kauli yake aliyoitoa juzi, jijini Dar es Salaam imeendelea kudhihirisha jinsi rushwa ilivyo mfupa mgumu ndani ya jeshi hilo kama na yeye alivyokiri.

Juzi, Rais Samia alisema licha ya jitihada zinazoendelea kufanyika kuliboresha Jeshi la Polisi bado rushwa imekuwa mfupa mgumu kwa jeshi hilo.

Utafiti uliowahi kufanywa na wa shirika lisilo la kiserikali la Twaweza na kutangazwa Novemba 23, 2017, ulibaini kuwa Polisi na Mahakama bado zinaongoza kwa rushwa, licha ya kuwa ni taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, wananchi wanaripoti kuwa licha ya viwango vya bado vya juu ndani ya Polisi na Mahakama. Kati ya asilimia 36 na 39 ya wananchi waliohojiwa, waliiambia Twaweza kuwa waliombwa rushwa mara ya mwisho walipofika katika taasisi hizo.

Wananchi walitoa maoni, walisema ili kupata huduma ya uhakika katika sekta hizo, lazima utoe rushwa.

Akizungumza (Septemba 4, 2023) wakati wa ufunguzi wa kikao cha maofisa waandamizi wa jeshi la polisi, Rais Samia alisema wananchi bado wanalalamikia rushwa hasa kwa askari wa barabarani.

“Wimbo wa polisi mzuri na leo (juzi) kabla ya kuja hapa nilifungua youtube nikausikiliza kisha nikaangalia jeshi langu na kujiuliza ingekuwa yanayoimbwa hapa ndiyo yanayotendeka tungekuwa na jeshi la malaika,” anasema Rais Samia na kuongeza;.

Ukiachana wimbo na slogan yenu nzuri sana, lakini je mnayatekeleza? IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) naomba sana simamia utekelezaji wa wimbo na slogan ili jeshi liwe na sifa ile ya kimataifa.”

Anaweka wazi kwamba tatizo la rushwa kwa askari wa barabarani litapatiwa ufumbuzi baada ya uwekezaji kufanyika kwenye teknolojia.

“Wakati mwingine ni vigumu kubadilisha tabia, lakini inaweza kurekebishika kukiwa na teknolojia inayolazimisha watu wafuate teknolojia inavyotaka.

“Mfano tukiweka kamera za barabarani hakutakuwa na sababu ya askari kusimama barabarani kusimamisha magari, teknolojia itatoa mwongozo wa kila kitu na rushwa haitakuwepo,” anasema.

Rais Samia anafafanua uwekezaji huo ukifanyika kwenye teknolojia itasaidia kupunguza idadi ya askari barabarani na itawezesha kupatikana wa kwenda kwenye maeneo mengine yenye uhitaji.

Matamanio ya Rais Samia, wa kutaka kufunga kamera kunaungwa mkono na wananchi mbalimbali waliotoa maoni yao mitandaoni kuhusiana na kauli hiyo ya Rais.

Mmoja wa wananchi, aliyejitambulisha kwa jina la Ally Shaban, alisema Polisi wa pale Kitonga, Ruaha Mbuyuni na kwenye kizuizi Iringa baadhi yao wanatia aibu kwa vitendo vya rushwa.

“Baadhi ya askari wanadhani wapo pale kwa ajili ya kupokea rushwa na sio kuhudumia raia,” alisema Shaban na kuongeza; “Wakati mwingine wanalazimisha mpaka wapewe rushwa.”

Kwa mujibu wa mwananchi huyo, madereva wenyewe hulazimika kutoa rushwa ili kuepuka faini kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani kwa makusudi.

Mwananchi mwingine, John Paul, alisema Polisi hasa wa usalama barabarani wanategatega barabara nzima? wanaenda kupiga rushwa, kwani wanajua hakuna kamera.

“Nimepita Lugalo pale maofisa wameacha kukaa ofisini, wamekuja kuziokota barabarani maana ofisini hazifiki,” alisema mwananchi huyo.

Alisema trafiki hawawezi kukubali kamera, maana kuzikubali ni sawa na kuridhia wafe njaa, lazima fitna Ipigwe ili mpango huo wa Rais Samia usifanikiwe.

Mwananchi mwingine (jina linahifadhiwa) alisema kamera hizo hazitaondoa kabisa tatizo la rushwa kwa askari, ingawaje litasaidia kupunguza kwa kiasi fulani.

“Wasifunge kamera barabarani na/au mitaani tu, bali kila askari Polisi anapokuwa kazini iwe lazima avae kamera mwilinimwake, yaani Body-Camera (BodyCam) kama vile walivyo Askari Polisi wa Marekani.

Hii itasaidia kurekodi matukio yote yamhusu askari huyo wakati akiwa katika majukumu yake ya kazi sambamba na kuweza kufuatilia mienendo ya maaskari Polisi kwa urahisi na kuweza kuwabaini wale Askari Polisi ambao watajihusisha na matukio ya uhalifu.

Iwe ni sharti la lazima kwa Askari Polisi kuvaa BodyCam awapo kazini, ili kuwadhibiti askari Polisi wahalifu ambao wamekuwa wakilichafua Jeshi la Polisi, BodyCam iwe mojawapo ya Sare za Askari Polisi awapo kazini,”anasema.

Mwananchi mwingine, Edgar Swai, anasema Polisi wa Usalama barabarani wanakera mpaka basi. “I wish wangeondolewa kabisa barabarani.

Wengi wao wanapenda sana rushwa,” anasema.
Alisema kwa makosa ya mwendo kasi na bima itakuwa ni vuziri kutumia kamera, lakini hadhani kama kamera pekee yake zitaweza kufanya ukaguzi wa ubora wa magari, kukagua mizigo na mengineyo.

“Bado watahitajika askari kwa ajili ya ukaguzi wa magari. Labda ukaguzi kama huu pia ufanyike sehemu ambazo zina kamera pia

Hizo kamera si zitasimamiwa na watu au zitajiendesha zenyewe? Polisi watazichezea tu. Ni vizuri kila basi iwekwe namba ya simu ya kamanda. Abiria akihisi kuna rushwa anapiga simu kwa kamanda nakala kwa Takukuru,”alisema.

Naye Bejamini Netanyahu alisema kwa hilo anaunga mkono zifungwe kamera za usalama ama rada hii itaondoa rushwa kwa asilimia 100.

Anadai kwamba wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tatu, ubalozi wa China ulitoa kamera za kufungiwa barabarani kwa jeshi la polisi, lakini hizo kamera hazikuwahi kufungwa na hakuna mtu aliyewahi kuhoji.

Mwingine anasema trafiki aliowaona Arusha hajapata kuona popote, kila baada ya kilomita moja unakuta kundi la askari. Mwingine, anasema zikifungwa kamera kuna watu watakufa kwa hilo ,maana kuna trafiki wamejenga nyumba kwa rushwa.