December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanza yaanika mafanikio miaka 63 ya uhuru

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza


MKOA wa Mwanza,umetaja mafanikio yaliopatikana katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ya kiuchumi,kisiasa na kijamii,ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.

Akizungumza katika maadhismisho ya siku ya Uhuru wa Tanganyika yaliofanyika kimkoa wilayani Ilemela,Desemba 9,2024,Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai,amesema Mkoa wa Mwanza umeimarisha miundombinu ya barabara.

Ambapo barabara za lami zimeongezeka kutoka km 8.81 mwaka 1961 hadi km 359.895 mwaka 2024, huku barabara za changarawe zikiongezeka kutoka km 125 hadi km 2,213.

Zaidi ya hayo, huduma ya maji safi imeongezeka kwa kiwango kikubwa, na sasa asilimia 70 ya vijiji vya Mkoa vinapata huduma hiyo, ikilinganishwa na vijiji vichache vilivyokuwa na maji safi mwaka 1961.

Ngubiagai amesema, katika sekta ya afya, vituo vya afya na hospitali vimeongezeka kutoka tatu hadi 27 zikiwemo Hospitali za Rufaa za Sekou-Toure na ya Rufaa ya Kanda Bugando, inayotoa huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi,pia Mkoa umejenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa mpya Nansio.

Aidha, amesema Mkoa umeongeza idadi ya zahanati kutoka 14 hadi 371,sekta ya elimu pia imeonesha maendeleo huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka tano mwaka 1961 hadi kufikia shule 332,mwaka 2024.

Uchumi wa Mkoa umeimarika kupitia viwanda, viwanda vikubwa vimeongezeka kutoka vichache vya kuchambua pamba hadi kufikia 64, vya kati 171 ambapo uwekezaji katika sekta ya umeme umewezesha vijiji vingi kupata umeme,vijiji 23 sasa vipo katika mpango wa kupata umeme wa jua.

Ngubiagai ameeleza kuwa maendeleo hayo ni matokeo ya uongozi madhubuti wa Serikali katika awamu mbalimbali, na ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa sera za maendeleo.

Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo kwa manufaa ya vizazi vijavyo, na akaahidi kuendeleza mafanikio hayo kwa kuzingatia maono ya waasisi wa taifa.

Kauli mbiu ya sherehe hizo, “Miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika,”Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo Yetu,” imekumbusha umuhimu wa mshikamano, uongozi bora, na juhudi za pamoja katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.