December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia apongezwa kwa kudumisha amani

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Tabora

RAIS Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kusimamia vema tunu ya amani na utulivu wa nchi na kuwezesha wananchi kuendelee kufurahia matunda ya Uhuru wa Taifa lao.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Said Nkumba,wakati akizungumza  na Majira juu ya matunda ya miaka 63 ya Uhuru, ambapo amesema cha kujivunia kwenye nchi ni uhuru na amani.

“Amani na utulivu ni tunu iliyoasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Serikali zote zilizotangulia zimeendelea kuenzi tunu hiyo kwa vitendo,”.

Nkumba amesema tangu Rais Samia amekuwa kinara wa maendeleo na ameunganisha watanzania wote pasipo kujali itikadi zao za kisiasa, kabila wala dini, na ameendelea kuwahakikishia usalama wao na mali zao.

‘Tunampongeza sana Rais Samia  kwa kudumisha demokrasia hapa nchini na kutoa fursa kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa kufanya shughuli zao kikamilifu pasipo kuvuruga amani ya nchi,’ alisema.

Amesema ushiriki wa vyama vyote vya siasa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliomalizika hivi karibuni hapa nchini ni ushahidi tosha kuwa Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na CCM imedumisha demokrasia.

Nkumba amesisitiza kuwa hata maeneo ambayo vyama vya upinzani vimeshinda ni ushahidi tosha kuwa wananchi wana haki ya kuamua nani awe kiongozi wao kupitia karatasi ya kura na atakayeongoza kwa kura ndiye atakuwa kiongozi wao.

Akizungumzia mafanikio chanya yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru,amesema kuwa Watanzania sasa wanatembea kifua mbele kutokana na kuboreshwa kwa huduma za kijamii katika halmashauri zote nchini.

Ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuboreshwa huduma za afya kwa kujengwa zahanati, vituo vya afya, hospitali za Wilaya, Mikoa na Rufaa, hii imesaidia kumaliza au kupunguza kero ya upatikanaji huduma za afya nchini.

Mengine ni kuboreshwa miundombinu ya barabara na kujengwa barabara za lami, shule za kisasa, umeme kila kijiji na kitongoji, wananchi kuwezeshwa mikopo na serikali na kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa-SGR.

Aidha aliongeza kuwa ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi umeongezeka sana kutokana na mazingira wezeshi ambayo yameendelea kuwekwa na serikali, ongezeko la wawekezaji na jamii kuanzisha maduka na vibanda vya biashara ni matunda ya amani na utulivu uliopo nchini.