December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050 kuzinduliwa

Na Imma Mbuguni, TimesMajira Online, Dar es Salaam

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kuzindua rasmi rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ikiwa ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya dira hiyo, katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar. Uzinduzi huu utahudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali, wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye atakuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ijumaa, Desemba 6, 2024.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Prof. Mkumbo alisema kwamba uzinduzi huu unafuatia zoezi la kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na wadau wa maendeleo, ambapo jumla ya watu 1.17 milioni walishiriki kupitia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tafiti za kaya, mahojiano, makongamano, na ujumbe wa simu (USSD).

“Uzinduzi wa Rasimu ya Dira 2050 utakwenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya kukusanya maoni, ambayo itahusu uhakiki wa Rasimu ya Dira 2050. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa inazingatia maoni na mapendekezo kutoka kwa wananchi na wadau wote,” alisema Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo alifafanua kuwa baada ya zoezi la uhakiki, rasimu iliyoboreshwa itapokelewa na Waziri Mkuu Januari 18, 2025. Aidha, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itajadiliwa na vyombo mbalimbali vya serikali, ikiwa ni pamoja na Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango, na Baraza la Mawaziri, kati ya Januari na Machi 2025. Hatimaye, rasimu hiyo itajadiliwa na kuidhinishwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Aprili na Mei 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Mei au Juni 2025. Uzinduzi huu utakuwa ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya taifa.

Prof. Mkumbo aliongeza kuwa maandalizi ya Dira 2050 yanaenda sambamba na maandalizi ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Maendeleo (Long-Term Perspective Plan – LTPP), utakaotafsiri maono na matamanio yaliyopo katika Dira 2050.

“Dira hii ni ya Watanzania wote. Tunawaomba Watanzania washiriki kikamilifu katika hatua zote za mchakato huu hadi siku rasmi ya uzinduzi,” alisema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Bw. Deodatus Balile, aliishukuru serikali kwa kujumuisha vyombo vya habari katika mchakato wa kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa serikali na vyombo vya habari katika kutoa taarifa kwa wananchi na kusikiliza maoni yao.

“Lazima tuwe na utamaduni wa serikali kuwafikishia wananchi taarifa, na pia serikali kupokea taarifa kutoka kwa wananchi. Hii ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Balile.

Aliendelea kusema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inapaswa kuwa chombo kinachounganisha Taifa, kikiwa na muktadha wa kuhakikisha kuwa mabadiliko yoyote ya viongozi hayaathiri vipaumbele vilivyowekwa katika Dira hiyo.
“Hili ni jambo muhimu kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu.

Ili tuweze kulipeleka mbele, Dira hii inapaswa kuwa na mwelekeo wa pamoja, unaohusisha sekta zote muhimu kama vile viwanda na elimu bora,” alihitimisha Balile.

Uzinduzi wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unatarajiwa kuwa ni tukio muhimu katika mchakato wa kuhakikisha kuwa taifa la Tanzania linapata mwelekeo na mikakati endelevu ya maendeleo katika miaka ijayo.