Ni katika mazungumzo na marais mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa, WB yaahidi neema katika miradi, imo SGR
Na Mwandishi Wetu, aliyekuwa Rio di Janeiro
TANZANIA imepata manufaa makubwa kutokana na ushiriki wake katika mkutano wa viongozi wa nchi zenye uchumi mkubwa zaidi zijulikanazo kama G20.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishiriki mkutano huo muhimu uliomalizika nchini Brazil, ikiwa ni pamoja na kufanya vikao vya pembeni (uwili) na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa baadhi ya nchi pamoja na mashirika ya kimataifa.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliweka wazi mafanikio makubwa ambayo Tanzania itapata kutokana na mikutano hiyo ya pembeni (uwili), wakati alipoulizwa kuhusu manufaa ambayo Tanzania itapata kwa kushiriki kwake katika mikutano ya uwili, wakati alipohudhuria Mkutano wa G20 uliofanyika Jiji la Rio di Janeiro.
Rais Samia alieleza manufaa hayo wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari alioambatana nao kwenye ujumbe wake.
“Ukiangalia watu niliokutana nao kwenye side meetings (mikutano ya uwili) huwapati kwenye plenary (mkutano wenyewe), unawapata kwenye nikutano ya pembeni ambapo kwa Tanzania tumefaidika sana.” Alieleza Dkt Samia
“Kati ya Marais ambao nilikutana nao ni Cyril Ramaphosa, wa Afrika Kusini. Ambapo kwanza lengo lilikuwa ni kumpongeza kwa uchaguzi wa kwao, ulikuwa mgumu kidogo, lakini alisimama amechagua viongozi wa kufanya nao kazi kuunda Serikali na sasa wanakwenda vizuri.”
Lakini la pili ni kumpongeza kwa kuwa mwenyekiti wa G20 mwakani, jambo kubwa sana maana kwa watu wale ni vigumu kumwamini Mwafrika awe Mwenyekiti wao, ni jambo kubwa sana,” alisema Samia.
Mkutano wa G20 mwaka 2025, unatarajia kufanyika nchini Afrika Kusini chini ya Mwenyekiti ambaye ni Rais wa nchi hiyo, Cyri Ramaphosa ikiwa na kaulimbiu “Kuendeleza Umoja, Usawa, na Maendeleo Endelevu”
“ambayo yote kwa Mwafrika ndio shughuli yetu. Na hivyo kumuhakikishia utayari wa Tanzania kumsaidia katika jukumu lake Uenyekiti wa G20.” Alisema Rais Samia
Viongozi wengine aliokutana nao ni Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store, ambapo walijadiliana na kukubaliana kuendeleza mikakati ya kuhakikisha Afrika inapata umeme wa kutosha, kwani Norway ni mshirika mkubwa na muhimu katika masuala ya nishati.
Rais Samia pia alikutana na Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi ambapo pamoja na mengi waliyozungumza, mradi wa bwawa la umeme la Mwalimu Julius Nyerere ulijadiliwa, pamoja na mkazo mkubwa kuwekwa katika matumizi mazuri ya maji ya Mto Nile ambapo wanaomba nchi zinazopakana na mto huo kuutumia vizuri ili Misri iendelee kunufaika na mto huo.
“Nilikutana pia na Waziri Mkuu wa Vietnam tulizungumzia miradi ya pamoja haswa mradi wa Halotel, ambao ulikuwa na matatizo ya hapa na pale , lakini tumemaliza, walikuwa na kesi mahakamani na tumemaliza vizuri na upande wao wanashukuru, lakini pia kuangalia maeneo mengine ya uwekezaji.” Alisema Rais Samia.
Wengine ni Indonesia ambao Tanzania ina ushirikiano katika miradi ya mafuta na gesi ambapo pia wanafuatilia mradi wa LNG, ambapo tayari pia Tanzania ina mikataba ya biashara iliyowahi kusainiwa hivyo kuona jinsi ushirikiano wa kuiendeleza itakavyotekelezwa, lakini pia ziara za wafanyabiashara kuja nchini na kutembelea Indonesia.
“Kwa kuwa Rais wa Indonesia ni Rais mpya ametuhakikishia uhusiano ulioanzishwa na mtangulizi wake utaendelea na kwamba atakapofanya ziara katika nchi za Afrika, atatembelea Tanzana.” Alisema Rais Samia.
Katika mikutano hiyo ya pembezoni, Rais Samia pia alikutana na viongozi wa Benki ya Dunia (WB) pamoja na Benki ya Afrika(AFDB) ambapo pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa ni Mkutano wa Nishati unaofanywa kwa kushirikiana na taasisi hizo, utakaofanyika Januari 2025, nchini Tanzania.
“Kwa hiyo tunaangalia mikakati ya kufanikisha hilo. Lakini Benki ya Dunia wametuhakikishia bodi ikishakaa siku zijazo watatupa pesa za miradi mbalimbali ambayo ni pamoja na SGR” alisema Rais Samia
Katika mikutano ya uwili, Rais Samia alikutana na uongozi wa taasisi ya Asia Infrastructure ambayo ni taasisi ya nchi za Asia, ambayo pia wanatoa uanachama kwa nchi nyingine.
“Hivyo Tanzania tumeona umuhimu wa kuingia kwa kuwa benki hiyo inasaidia ujenzi wa miundombinu, fedha za ujenzi wa miundombinu.” Alisema Rais Samia.
“Kwa kifupi ukiangalia watu niliokutana nao kwenye “side meetings” huwapati kwenye “plenary”, wapo zaidi katika mikutano hiyo ambapo kwa Tanzania tumefaidika sana. Mathalani yule mliyeahidiana anaweza asitekeleze, lakini mkionana uso kwa macho anakwenda kulimaliza na pesa zinatoka.
Kwa hiyo tumefaidika kwa kwenda kuonana nao hao wote”.
More Stories
Wahitimu waliosoma MNMA washauriwa kutumia kusanyiko kutoa maoni ya kuendeleza chuo
Viongozi wa mitaa Korogwe TC watakiwa kusimamia maendeleo ya wananchi
VETA yaja na mbinu kutatua changamoto sekta ya ukarimu na utalii