November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA.Makalla:Kesho tuungane na Rais kupiga kura

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline. Morogoro

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM) Taifa, CPA. Amos Makalla, amewaomba wananchi wote hususani wanachama wa CCM, kesho Novemba 27, mwaka huu kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenda kupiga kura.

CPA. Makalla ameyasema hayo leo Novemba 26, 2024 katika Jimbo la Mikumi mkoani Morogoro, alipokuwa kwenye Mkutano wa Hadhara wa Ufungaji wa Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Chama hicho, huku akiwasisitiza wananchi kuwa, kupiga kura ni haki muhimu kwa kila Mtanzania.

Amesema ni vyema kesho kila mmoja akaenda kutimiza wajibu wake wa kuchagua viongozi watakao waletea maendeleo na kusema kuwa viongozi hao wanatoka CCM.

Pia amesema kuwa, CCM ndiyo Chama pekee kilichosimamisha mawagombea kwa asilimia 100, tofauti na vyama pinzani, huku akidai kuwa ndiyo sababu ya kufeli kwa vyama pinzani katika mchakato mzima wa ufanyaji kampeni.

“Niwaombe wote kesho tukatumie haki yetu ya msingi ya kwenda kupiga kura na kuwachagua wale wagombea wanaofaa kwa ajili ya maendeleo yetu, hivyo nawaomba kesho tukamuunge mkono Rais wetu kupiga kura katika sehemu zetu, ambapo yeye kesho atakuwa Chamwino mkoani Dodoma ndipo atakapo pigia kura.

Niwaombe tukakipigie kura kwa wingi chama Cha CCM kwani ndiyo chama pekee kilichosimamisha wagombea kwa silimia 100 tofauti na wenzetu wao walikuwa wanaruka ruka na ndiyo maana wameshindwa hata katika kampeni zao”, amesema Makalla.

Pia, amewaomba wanaccm kuondoka maeneo ya kupigia kura pindi wanapomaliza kupiga kura huku akisema kuwa, kuendelea kubaki katika vituo hivyo kwa madai ya kulinda kura ni ishara ya kutojiamini.

“Nimewasikia wale wanaojiita Makamanda wanasema tukimaliza kupiga kura tusiondoke katika vituo tusubiri, huo ni ukorofi, sisi wanaccm tukimaliza kupiga kura niwaombe turudi majumbani kwani CCM tunajiamini na tunaamini tutashinda kwa kishindo”, ameongeza Makalla.

Sambamba na hayo, Makalla amewaomba wakazi wa Mikumi Mkoani Morogoro kumuombea aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule maarufu Prof. J kuimarika kiafya huku akiwataka kutochanganya maombi yao kwa kumuombea kura katika kijiji.

“Tumuombee Prof J apone huo ndiyo ubinadamu kila mmoja amuombe kwa dini yake ila msichanganye maombi kwa kumuombea apate Kijiji hata kimoja, msichanganye maombi kwa Mungu..ubinadamu tumefanya kumuombea apone na arudi na afya njema,”amesema Makalla