November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KUELEKEA uchaguzi wa serikali za mitaa waandishi wa habari Jijini Mbeya wametakiwa kutoa taarifa sahihi pamoja na kuepuka kuandika habari zenye kupotosha jamii na kuchochea ambazo zinaweza kuleta taharuki.

Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 23,2024  na Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)Benjamin Kuzaga wakati wa mafunzo ya waandishi  habari na maafisa wa jeshi la polisi kuhusiana na uchaguzi wa serikali za mitaa .

“Dhumuni kubwa ni kuwaomba kushirikiana na jeshi la polisi katika shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kuhabarisha wananchi wa mkoa wa Mbeya na maeneo mengine katika kuzingatia  mambo muhimu ili muweze kuwa  salama ikiwemo kutoa taarifa sahihi,kuepuka taarifa zenye kupotosha au kuchochea ,kuleta taharuki kwa jamii kama mnavyojua na nyie wanahabari mna taratibu na miongozo kwenye uandishi wenu wa habari ,pia vyombo vyenu vya habari mnavyoandikia hakikisheni  taarifa zinakuwa nzuri na kuhakikisha mnashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ili msiweze kuandika habari za kupendelea chama fulani “amesema Kuzaga.

Aidha Kuzaga amewataka waandishi wa habari kuwa na mipaka ya utoaji wa taarifa kwani chombo ambacho kinatambua kwamba kinatakiwa kutoa taarifa kwa undani zaidi sio mwandishi bali ni tume ya Taifa ya  Uchaguzi na kwamba polisi na waandishi ni watu pili kupata taarifa na taarifa sahihi inapatikana tume ya taifa ya uchaguzi.

“Kama utapata nafasi ya kuhoji na tume ikakupa kile ambacho unatakiwa naamini kabisa utaandika vizuri iwapo utaandika nje na yale ambayo tume imepanga kwa vyovyote naamin utaenda kinyume na tume kushindwa kukuelewa ,hivyo niwaombe kamwe msiwe watoaji wa taarifa za tume kabla tume haijapitia taratibu na kanuni zilizowekwa”amesema Kamanda Kuzaga.

“Tunategemea kila mmoja atafanya kazi kwa weledi na kutumia taaluma ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kuhabarisha umma jambo ambalo litapelekea uvunjifu wa amani” alisema Kamanda Kuzaga.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa  Mbeya (MBPC),Nebart Msokwa amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo kwa jitihada mbalimbali za kuzuia na kutokomeza uhalifu hali inayopelekea wananchi kuishi na kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.

Aidha Msokwa amelipongeza Jeshi la Polisi kwa ushirikiano linaloutoa kwa waandishi wa habari na kusisitiza kuendelea kushirikiana, kufanya vikao na mafunzo ya mara kwa mara ili kukumbushana masuala ya kiutendaji ikiwemo sheria na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Kwa upande wake Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kinyongo ameeleza kuwa, Jeshi hilo limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama kabla, wakati na baada ya uchaguzi na kuwaomba wananchi kutokuwa na hofu yoyote na kwenda kwenye vituo vya kupigia kura Novemba 27, 2024 ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura kuwachagua viongozi ngazi ya Mitaa, Vitongoji na Vijiji.