Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dar
HOSPITALI ya CCBRT imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi kwa kutoa huduma ya matibabu ya macho kwa wagonjwa zaidi 1,000 na wengine 200 wa rufaa wamepimwa na kupatiwa matibabu katika zoezi linaloratibiwa na Hospital ya CCBRT katika kambi tatu tofauti Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi habari Jijini Dar es Salaam leo wakati maandalizi ya kambi ya upimaji macho kwenye shule za msingi za Mzambarauni na Amani zilizopo Ukonga ambako zoezi hilo lilifanyika jana baada ya lile lilofanyika kwa mafanikio makubwa kwenye Kambi ya Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa Novemba 9,2024, Dkt Sunguro Chacha alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa sana.
“Zoezi la upimaji macho kupitia kambi hii limekukuwa na mafanikio makubwa kwani tumeweza kubaini wagonjwa wengi wenye matatizo na kuwapa matibabu, ushauri na wengi kuwapa rufaa ya matibabu zaidi kwenye hospitali yetu iliyopo eneo la Msasani,” alisema Dkt Sunguro.
Dkt Sunguro ambaye aliambatana na Dkt Maxine Michael Harker wote kutoka Hospitali ya CCBRT alisema kambi hiyo ya siku tatu imeandaliwa kwa ushirikiano wa Hiospitali ya CCBRT na Shirika linalohusika na huduma za macho lilojulikana kama Light For The World (LFTW).
Naye Mratibu wa Kambi hizo kutoka Hospitali ya CCBRT, Mariam Mchomvu, alisema uhamasishaji mkubwa umefanywa na unaendelea mitaani ili wananchi zaidi wenye matatizo ya macho wajitokeze kupima afya ya macho ili kubaini tatizo mapema na waweze kupata matibabu.
“Zoezi hili la siku tatu litahitimishwa kesho kwenye kambi iliyopo Shule za Msingi Mbagala Rangi Tatu na Mchikichini zote zipo Mbagala Rangi Tatu,” alisema Mariam na kuongeza kuwa sambamba na zoezi hilo timu ya wataalamu kutoka CCBRT inapata fursa ya kuwabaini akina mama waliopata changamoto baadaya kujifungua (Fistula).
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Deo Joseph mbali ya kuishuru Hospitali ya CCBRT, ameipongeza pia kwa kutafsiri kwa vitendo 4R za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuifanya shule yake kuwa kambi ya kudumu ya upimaji macho.
“Hii ni mara ya pili shule yangu kufanywa kambi ya upimaji macho na watoto wangu ni wanufaika wa kwanza wa huduma hii. Zoezi hili limekuwa na faida kubwa siyo kwa watoto pekee bali pia kwa jamii nzima inayotuzunguka,” alisema Mkuu wa Shule huyo Joseph.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliojitokeza kupima macho, Said Mwakifwamba ambaye pia ni mfanyabiashara wa matunda Kariakoo aliishukuru Hospitali ya CCBRT kwa kutoa huduma ya upimaji macho bure na matibabu yake kwa wale waliobainika kuwa na matatizo.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika